Habari za Punde

Wizara ya Afya yakabidhiwa msaada wa mashine za kupumulia

Baadhi ya Mashine za Kupumulia alizokabidhiwa Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii , Wazee, Jinsia na Watoto Mhe, Nassor Ahmed Mazrui,  zilizotolewa Msaada na Shirika la World Federation Of Khoja Shia Ethna Asheria Muslim Communities, Hafla iliyofanyika Wizarani Hapo Mjini Zanzibar.
Dkt. Jaffer Dharsee (Kulia)  Kutoka Shirika la World Federation Of Khoja Shia Ethna Asheria Muslim Communities, akimkabidhi Msaada wa Mashine 50 za Kupumua Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii , Wazee, Jinsia na Watoto Mhe, Nassor Ahmed Mazrui, na wakwanza (Kulia ) ni Mkurugenzi Tiba wa Wizara hiyo, Dkt. Amour Suleiman Mohamed , Hafla iliyofanyika Wizarani Hapo Mjini Zanzibar.
 Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii , Wazee, Jinsia na Watoto Mhe, Nassor Ahmed Mazrui, akizungumza baada ya kukabidhiwa Msaada wa Mashine 50 za Kupumua, kutoka Shirika la World Federation Of Khoja Shia Ethna Asheria Muslim Communities,Hafla iliyofanyika Wizarani Hapo Mjini Zanzibar.

(PICHA NA MARYAM KIDIKO – MAELEZO ZANZIBAR )


Na Rahima Mohamed Maelezo 06/01/2022

Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto imepokea msaada wa mashine (50) hamsini za kupumulia kutoka Shirika la Jumuiya za Kidini World Federation ili kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo hayo.

Akipokea msaada huo Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Nassor Ahmed Mazrui huko Ofisini kwake Mnazi Mmoja Mjini Unguja, amesema mashine hizo ni muhimu sana ambazo zitarahisisha utoaji wa huduma katika kipindi hiki jamii imekumbwa na maradhi mengi ya kupumua.

Amesema matatizo ya kupumua ni hatari sana hivyo mashine hizo zitasaidia kuokoa maisha watu wenye matatizo mbalimbali wakiwemo wajawazito, watoto pamoja na jamii kwa ujumla ambao wanahitaji huduma hiyo.

Waziri Mazrui mashine hizo zitaipunguzia gharama Serikali ya kusafirisha mitungi ya oxygen kutoka hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na kwenda hospitali nyengine ili kutoa huduma hiyo.

Akikabidhi mashine hizo Dk. Jaffer Dharsee kutoka shirika la World Federation amesema shirika lake linatoa huduma mbalimbali za jamii ikiwemo sekta ya afya ili kunusuru maisha ya wananchi.

Aidha ameishukuru Wizara hiyo kwa mashirikiano mazuri yaliopo na kuahidi kuongeza mashine 35 pamoja na kusaidia mahitaji mengine katika uzalishaji wa gesi hiyo ili kupunguza usumbufu wa mahitaji hayo nchini.

Nae Mkurugenzi Tiba Amour Suleiman Moh’d amesema mashine hizo zitagaiwa katika hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye shida ya kupumua na kiwango kidogo cha hewa ya oxygen mwilini.

Aidha amewataka watendaji wa huduma za afya  kuzitumia vizuri mashine hizo na kuhakikisha kwamba wanazitunza ili kuepuka hitilafu zitakazopelekea uhaba wa uzalishaji na upatikanaji katika hospitali na vituo vya afya nchini.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.