Habari za Punde

SERIKALI KUNUSURU MTO MSIMBAZI

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni jijini Dodoma Februari 4, 2022.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa programu maalumu za kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu matumizi ya Mwongozo wa mita 60 kwa lengo la kunusuru mazingira ya vyanzo vya maji ikiwemo Mto Msimbazi.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis bungeni jijini Dodoma Februari 4, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Mhe. Bonnah Kalua aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wakulima wa mbogamboga pamoja na hatua za kuchukua ili kulinda mazingira katika Bonde la Mto Msimbazi. 

Mhe. Khamis alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeelimisha watendaji wa halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi wanaofanya shughuli za kimaendeleo kwenye bonde hilo kuzingatia kanuni na miongozo ya hifadhi ya mazingira.

“Serikali imebaini uharibifu wa mazingira ya Mto Msimbazi unaofanywa na wananchi wanapofanya shughuli si za kilimo tu bali pia uchimbaji wa mchanga pamoja na umwagaji maji machafu kwenye Bonde la Mto Msimbazi, kupitia Kifungu cha 57 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004, katika kuhakikisha kwamba wakulima wa mbogamboga pamoja na wadau wengine hawaharibu mazingira ya bonde hilo,” alisema.

Aidha, naibu waziri huyo alibainisha kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa programu maalum za kuelimisha na kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya Mwongozo wa mita 60 kwa lengo la kunusuru mazingira ya vyanzo vya maji ikiwemo Mto Msimbazi.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mabalozi wa mazingira imeanza utekelezaji wa Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira ambapo suala la hifadhi ya vyanzo vya maji ni moja ya eneo la kipaumbele katika utekelezaji wa kampeni hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.