Habari za Punde

Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuhamasishana juu ya kupinga matendo maovu nchini.

 

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipojumuika na wanamazoezi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika mazoezi ya yaliyoanzia Chakechake Benki  na kumalizia Uwanja wa Gombani.

Amesema vikundi hivyo vina ushawishi mkubwa katika jamii kwa kuwafikia rika zote ni vyema kutumia vikundi hivyo kwa kuisaidia Serikali katika kupinga vitendo viovu ikiwemo Madawa ya kulevya na udhalillishaji wa wanawake na watoto.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwataka wana mazoezi hao kueleza mazuri yote yanayofanywa na Serikali ili jamii iongeze uelewa zaidi juu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa wananchi wake.

Akigusia kuhusiana na umuhimu wa mazoezi Mhe. Hemed ambae pia ni mlezi wa vikundi vyote vya mazoezi Zanzibar amewataka wananchi kutenga muda wa kufanya mazoezi kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa Afya.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wanamazoezi hao kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu, sambamba na zoezi la utambuzi wa Anuani za makazi zoezi ambalo litasaidia Serikali kuweza kupanga mikakati yake pamoja kuwafikia wananchi wake kwa urahisi.

Kwa upande Wake Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mhe. Matar Zahor amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuweka kawaida ya kuungana na wanamazoezi nchini jambo ambalo linaamsha ari kwa wananchi juu ya kufanya mazoezi.

Kushiriki katika Mazoezi hayo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni Muendelezo wa utaratibu aliujipangia katika kuvitembelea vikundi vilivyopo Unguja na Pemba.
 
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.