Habari za Punde

KWAHERI INJINIA TATU ALLY

 

Na.Adeladius Makwega- DODOMA

Tuliingia katika mahojiano hayo ya kazi ya utayarishaji vipindi, watangazaji, mafundi mitambo, maafisa utumishi, wahudumu na kazi kadhaa zilizotangazwa na TBC, wakati huo shirika hilo lilikuwa chini ya Mkurugenzi Tido Mhando

Nayakumbuka majina kadhaa ambayo yalishiriki katika mahojiano hayo kama Neema Mbuja, Jamali Hashimu, Chunga Ruza, Gervas Hubile, Musa Ally, Leah Mushi, Frank Bahati, Zabron Bugingo, Beatrice Kategile, Antony Masere na wengine wengi.

Kwa hakika mahojiano hayo yalifanyika kwa sehemu mbili kwa watangazaji na watayarishaji vipindi kwa watumishi wengine walifanya mara moja tu.

Sehemu ya kwanza ilikuwa ni maswali ya mdomo tu, mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa Mkurugenzi Mkuu Tido Mhando na alipokuwa akitoka nje aliimuachi kiti chake mama mmoja Mtanzania mwenye asili ya Ujerumani na Upogoro aliyefahamika kama Joyceline Lugora aliyekuwa Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala.

Viongozi wengine wa TBC iliyotoka RTD na TVT walikuwapo akina Ngalimecha Ngahyoma, dada yangu mpenzi Edina Rajabu, Suzana Mungi, Taji Liundi na wengineo.

Hatua ya pili ya mahojiano yalihamia studioni, hapo nilikutana na watu wanne mara tu nilipoingia studioni wote walikaa upande wa mitambo, hapa tulipatiwa karatasi mbili za kusoma habari moja ilikuwa ya lugha ya Kiingereza na nyingine ya lugha ya Kiswahili.

Nakumbuka watu hawa wanne walikuwapo siku hiyo ni  Injinia Silvanus Haule (Huyu ndiye Injinia aliyerekodi nyimbo nyingi za  bendi za zamani, wimbo mmojawapo ni Dada Asha wa Tabora jazz wakati wa RTD miaka 1970), Aisha Dachi ambaye alikuwa Mkuu wa Idhaa ya TBC taifa wakati huo, fundi mitambo Josephy Masanja na Injinia mwingine Bi Tatu Ali .

Hapo tulikutana na watu watatu wa ufundi mainjinia wawili Silivanus Haule na Tatu Ally na fundi mitambo Josephy Masanja na naye Aisha Dachi yeye alikuwa ni mtu wa maudhui tu kutoka utayarishaji wa vipindi. Hao wote walioshinda mahojiano hayo walikuwa kweli watangazaji japokuwa wengine waliondoka TBC baadae akiwamo Neema Mbuja, Zabron Bugingo, Jamal Hashimu na mwanakwetu.

Tulipoinigia katika chumba hicho ambacho kilikuwa ni Studio ya Mshikamano baadaye nilibaini ilikuwa ilitumika kurekodi kwaya, bendi za muziki na vipindi vingine vya redio hii.

Injini Tatu Ali ambaye alikuwa mama mmoja mrefu, mweupe na mcheshi kununa kwake ilikuwa ni msamiati uliofutika kifuani mwake alisema kuwa mwangu kutoka Iringa chukua karatasi hizo mbili uzipitia kwanza kabla hatujaanza kurekodi.

“Mwanangu kutoka Iringa, kaa kwa amani , ondoa wasiwasi, anza kusoma, umenisikia ? soma bila woga ehh .”

Nilijibu naam.

Alisema mwanangu kutoka Iringa kwa kuwa mwanakwetu wakati huo niliomba kazi hiyo nikitokea Iringa Vijijini. Huku karatasi aliyoshika  Aisha Dachi ikionesha anuani yangu ya Iringa.

Baadaye nilikuja kumfahama kuwa Injinia Tatu Aliy alikuwa akishiriki kwa karibu kuisimamia Studio ya Mshikamano huku kwa karibu akishirikiana na Watayarishaji wa Vipindi vya Dini ya Kiislamu na Kikristu waliokuwa wakitoka BAKWATA, CCT na TEC.

Kwa wakati huo nakumbuka majina kama Padri Revokatus Makonge, Padri Anatory Salawa, Mchungaji John Magafu, Mchungaji John Kamoyo na Ustadh Mtahimbo Kislaa, Alhadj Musa Salumu wakitayarisha vipindi hivyo vya dini.

Kwa hakika watayarishaji hawa walikuwa wajuzi wa maudhui ya dini zao kwa hiyo Injini Tatu Ally alishiriki kwa sehemu kubwa kuzisanifu sauti za viongozi hao wa dini ili zisikike vizuri bila ya kujali kuwa kipindi kinachokwenda kurusha si cha dini yake.

Nakumbuka mara nyingi sana aliweza kurekodi kipindi cha Inueni Mioyo, Kumekuchwa na Hii ni Kwaresima.

“Msimamzi wa Kipindi cha Hii ni Kwaresima kwa leo ni Gervas Hubile, Mitamboni ni Injinia Tatu Ally na mimi ni Padri Anatory Salawa-Kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.”

Hapo Kipindi cha Hii ni Kwaresima kilikuwa kinafika tamati.

“Haya jamani asalaam aleikuum ! Namtafuta ustadhaat Injinia Tatu Ally yupo wapi?”

Niliwahi kumsikia Shekhe Mtahimbo Kislaa akiuliza.

Mwanakwetu hayo yote ninayasema leo hii kwa kuwa Injinia Tatu Ally amefariki dunia, baada ya kustaafu na Shirikia hilo la Utangazaji Tanzania miaka kadhaa iliyopita. Binafsi natoa pole kwa ndugu jamaa zake wote wa Dar es Salaam na Singida.

Nimejulishwa kuwa anazikwa Machi 3, 2022 huko mkoani Singida. Nimeyaandika haya kwa heshima ya Injinia Tatu Ally kwa yale niliyoyashuhudia kwa macho yangu. Natambua wapo wengi walioshuhudia mema mengi ya mama huyu.

“Dada Tatu Ally leo umelala, Mungu amekuita ukaitika, Injinia umekwenda rafiki yangu, daima nitakumbuka kwa uchesi na upendo wako, wana TBC tunakulilia, watoto wako wanakulilia. INALILAH WAINAHILAH RAJOUN.”

Haya aliyesema Hawa lilingani miongoni mwa watumishi wa TBC kwa sasa kutoka idara ya Ufundi ambayo injinia Tatu Ally alifanyia kazi kwa miaka mingi hadi kustaafu.

Binafsi namkumbuka mno, kwani hata fomu zangu za mikopo ya RTD Saccos alikuwa akinisainia kama mdhamini bila kugwaya.

Yote tunamuaachia Mwenyezi Mungu, atapima kwa haki yake.

Kwaheri Injinia Tatu Ally.

makwadeladius @gmail.com

0717649257

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.