Habari za Punde

Mhe Hemed ajumuika na waislamu katika Sala ya Ijumaa Masjid Hudaa, Maungani

Na Abdulrahim Khamis , OMPR

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na Waumini wa Masjid Hudaa Maungani Langoni katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Akitoa salamu kwa Waumini wa Msikiti huo Mhe. Hemed amewataka waumini na wananchi kwa ujumla kutoa mashirikiano ya kila hali ili kumaliza matendo maovu Nchini na kukemea tabia ya muhali inayoendelea katika jamii.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kuweka Sheria kali kwa wafanyaji wa matendo hayo  sheria ambazo zitakuwa ni funzo kwa wafanyaji wa matendo hayo na kupelekea kumaliza majanga hayo.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema umefika wakati kwa wazazi na walezi kulea na kusimamia  watoto katika malezi mema na kuwataka kurudi katika malezi ya kitamaduni ili kuirudisha Zanzibar katika malezi yaliyo mema.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed ameendelea kuwanasihi waumini hao kuendelea kuiombea Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi iweze kutimiza ahadi zake kwa wazanzibari na kueleza kuwa tayari jamii imeshajenga Imani kutokana na Miradi inayoendelea kujengwa ambayo itaweza kumaliza changamoto katika Jamii.

Akitoa Khutba katika Ibada hiyo Ustadh Is'haq Abbas amewataka waumini hao kusimamia majukumu yao hasa suala la kuchunga Familia zao jambo ambalo litapelekea kupata manufaa kwa M/Mungu Mtukufu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.