Habari za Punde

SMZ Itendelea Kutoa Ushirikiano Unaohitajika na Kujenga Mazingira Mazuri Ili Benki ya Biashara Tanzania (TCB) Kutoa Huduma Kwa Wananchi wa Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi akifungua mlango kuashiria ufunguzi wa Kongamano la Wanawake Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Biashara Tanzania Bw. Edmund Mndolwa (kushoto) kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki Jijini Zanzibar lililoandaliwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB).(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika na kujenga mazingira mazuri ili Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) iendelee kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar.

 

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akizindua Kongamano la Wanawake kuhusu Nafasi ya Mwanamke katika Kukuza Uchumi wa Buluu, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar ambapo Mama Mariam Mwinyi nae alihudhuria.

 

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa uwamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuunganisha benki ndogo ndogo zilizokuwepo awali kwa lengo la kuunda Benki ya TCB umelenga kuyanufaisha makundi mbali mbali ya wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali na wananchi kwa jumla.

 

Hivyo Rais Dk. Mwinyi aliihimiza Benki hiyo kufanya kazi kwa bidii na uzalendo ili malengo ya Serikali ya kuianzisha na kuiimarisha benki hiyo yaweze kufikiwa kwa maslahi mapana ya nchi.

 

Aliitaka benki hiyo kuongeza juhudi za kuwa wabunifu ili Taasisi hiyo isiyumbe, iendelee kuwa imara na yenye uwezo na nyenzo za kuhimili ushindani mkubwa uliopo ndani na nje ya nchi katika sekta ya huduma ya fedha. “Kuweni mstari wa mbele katika mageuzi ya kiuchumi yaliyopangwa na Serikali zetu katika pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”,alisema Dk. Mwinyi.

 

Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na taasisi za fedha pamoja na wawekezaji wa ndani na nje katika juhudi za kuendeleza uchumi wa buluu na kuhimiza kuzitumia kikamilifu fursa zinazotolewa na benki za hapa nchini.

 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi, alizihimiza Benki za hapa nchini kuendelea kushirikiana na wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo yenye unafuu wa riba na kuendela kuzisogeza huduma za fedha karibu na maeneo yao ya kazi,kuwapatia mafunzo pamoja na kuwapatia masoko.

 

Alieleza kuwa uwamuzi wa benki hiyo wa kutoa elimu na kuhamasisha wanawake kushiriki katika kutekeleza mipango inayohusu uchumi wa buluu ni muhimu ikizingatiwa kwamba uchumi wa buluu umejumuisha sekta kadhaa zikiwemo uvuvi, utalii, usafiri wa bahari, ujenzi wa bandari za kisasa, kilimo cha mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi na matumizi mengineyo ya rasiliamali za bahari kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

 

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi za kina mama katika kuendeleza zao la mwani ambalo ni sehemu ya uchumi wa buluu, hivyo kupitia kongamano hilo anaamini kwamba mipango na mikakati ya kuliendeleza zao hilo kwa matumizi ya mbegu bora pamoja na mbinu za kuliongezea thamani na utafutaji wa masoko itajadiliwa.

 

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea na jitihada za kuwapatia mitaji, vifaa na masoko wazalishaji wa mwani wa Unguja na Pemba kwani imeweka mkazo maalum wa kuyapatia mikopo makundi mbali mbali ya wanawake wanaojishughulisha na uzalishaji mwani na shughuli nyengine za biashara.

 

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuvutiwa kwake na uwamuzi na utaratibu wa Benki ya Biashara Tanzania wa kuweka mkakati maalum wa kuandaa na kuendesha makongamano malaum ya wanawake kwa ajili ya kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya wanawake kwa lengo la kustawisha ustawi wa wanawake nchini.

 

Nae Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuwakomboa wananchi kiuchumi na kusisitiza kwamba hatua zake hizo zitaendelea kuungwa mkono kwani ana nia njema ya kuwasaidia wananchi wake.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Dk. Edmund Mndolwa alieleza kwamba licha ya changamoto kadhaa inazozipata Benki hiyo lakini hata hivyo imeweza kupata mafanikio makubwa na kueleza matumaini yake kwamba benki hiyo ndani ya miaka mitano itakuwa ni beni ya mfano hapa nchini.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB),  Sabasaba Moshingi alieleza matumaini yake makubwa ya maendeleo yatakayofikiwa na Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.

 

Alisema kuwa Benki hiyo ya Biashara (TCB) ni Benki kongwe ambayo ina miaka 97 tokea kuanzishwa kwake na ambayo inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 83, Shirika la Posta Tanzania asilimi 8, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar asilimia 3, Posta na Simu asilimia 3 na Mfuko wa Hifadhi wa Jamii kwa watumishi wa Umma asilimia 2.

 

Katika hafla hiyo Rais Dk. Mwinyi alitoa zawadi mbali mbali kwa wateja wa benki hiyo vikiwemo vikundi vya wajasiriamali, Taasisi ya Maisha Bora  ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ pamoja na kukabidhiwa kadi yake ya uwanachama wa benki hiyo.

 

Mapema Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kukagua bidhaa mbali mbali za Wajasiriamali waliokuwepo hotelini hapo katika hafla hiyo.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.