Habari za Punde

makamuwa pili azindua shamrashamra za kutimia miaka 58 ya muungano

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati wa Uzinduzi wa shamrashamra za sherehe za maadhimisho ya Muungano wa Tanzania , uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza kuwa uwepo wa Muungano wa Tanzania kumepelekea kupatikana fursa mbali mbali kisiasa, kiuchumi na Kijamii.

Mhe. Hemed ameeleza hayo katika uzinduzi wa Shamra shamra za Maadhimisho ya kutimia miaka 58 ya Muungano na kumbukumbu ya miaka 50 ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume katika Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar. 

Amesema kuwa tokea kuasisiwa kwa Muungano wa Tanzania mwaka 1964 Watanzania wamekuwa wakipata fursa mbali mbali katika nyanja mbali mbali hasa muingiliano wa Kidamuna kiuchumi uliopo ambao umesababisha uwepo wa Idadi kubwa ya wawekezaji na wafanyabiashara ndani ya Tanzania. 

Amesema Serikali ya Awamu ya Nane ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia dhana ya Muungano ili kuuimarisha uzidi kukuwa kwa maslahi ya watanzania huku akigusia kuondoa hoja kumi na moja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman ameendelea kuwaeleza wazanzibari uhalali wa Muungano wa Tanzania na kuwataka kuendelea kuusoma vyema Muungano huo ili kujua historia ya Nchi yao.

Aidha Mhe. Hemed amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuitangaza Tanzania katika Mataifa mbali mbali jambo ambalo linakuza Diplomasia pamoja kutangaza mengi yaliyopo Nchini.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwataka wazanzibari kuenzi na kulinda jitihada za muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume ambae alijitoa kwa ajili ya wanzabari na kufanikisha kufanyika kwa Muungano wa Tanzania.


Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa uwepo wa Amani na utulivu Nchini ni moja kati ya faida kubwa za uwepo Muungano  ambapo amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kiuchumi kwa Amani iliyokuwepo.

Kwa upande wake  Kaimu waziri wa Nchini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Harun Ali Suleiman ameeleza kuwa uwepo wa  Muungano wa Tanzania ni tunu ya kipekee ambayo ni vyema kuendelea kuulinda ili Tanzania izidi kukuwa katika nyanja mbali mbali.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
20 Aprili 2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.