Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi awaasa wafanyabiashara kwenye risala yake ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan

 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                                                 1.04.2022

---

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amewanasihi wafanyabiashara wenye tamaa kutoutumia mgogoro wa Urusi na Ukraine kuwa ni kisingizio cha kupandisha bei za bidhaa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika risala yake ya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani  kwa mwaka 1443 Hijria sawa na mwaka 2022 Miladia, aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari nchini.

Amesema kuwa Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria wafanyabiashara watakaokwenda kinyume na maagizo inayoyatoa kwani amepata taarifa kwamba, bidhaa nyingi za vyakula zitakazouzwa kwa kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zimeingizwa  nchini  mapema  kabla  kuibuka kwa mgogoro  wa Urusi na Ukraine. 

Rais Dk.Mwinyi aliwahakikishia wananchi na wafanyabiashara kwamba Serikali itaendelea kufatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa dunia pamoja  na gharama za kufanya biashara duniani ili kuhakikisha kwamba  bei za  bidhaa mbali mbali zinazouzwa kwenye maduka ya jumla na reja reja zinaakisi uhalisia wa gharama pamoja na uwezo na kipato cha wananchi.

Aliwahimiza wakuu wa taasisi zinazoshughulika na biashara, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Masheha  wahakikishe kwamba wanafatilia kwa karibu mwenendo wa bei za  bidhaa mbali mbali katika maeneo yao ya utawala na  kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojaribu kukiuka sheria na maagizo yaliyotolewa na Serikali.

Katika risala yake hiyo, alisema kuwa wakati Mwezi Mtukufu wa  Ramadhani ukikaribishwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia bado hauko katika hali ya kawaida, kama ilivyokuwa kabla ya kuzuka kwa janga la UVIKO 19, mwishoni mwa  mwaka 2019.

Aliongeza kuwa pamoja na kuendelea kuwepo kwa changamoto zilizoambatana na maradhi hayo, hivi karibuni  mgororo  wa vita baina ya Taifa la Urusi na Taifa la Ukraine umeibua taharuki mpya kwa maendeleo ya  kiuchumi  na kijamii duniani kote.

“Serikali zetu zote mbili zinaendelea kufatilia kwa karibu matukio  hayo  na kuchukua hatua za tahadhari ili kupunguza athari zinazojitokeza katika uchumi wetu”,alisema Dk. Mwinyi.

Alieleza kuwa kwa kuzingatia hali ya uchumi nchini pamoja na uchumi wa dunia  kwa jumla amekuwa akiitisha vikao na watendaji wa taasisi mbali mbali za Serikali kwa lengo la kujadili maendeleo ya  biashara nchini ambapo amekuwa akitoa maagizo na maelekezo yenye lengo la  kudhibiti hali ya upandaji wa  bei za vyakula, mafuta ya petroli na bidhaa nyengine muhimu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa kipindi cha Mwezi wa Ramadhani, Serikali imepunguza viwango vya kodi kwa bidhaa muhimu za vyakula ambapo maamuzi yaliyofanywa katika suala hili yamezingatia maslahi ya wananchi pamoja na wafanyabiashara ambapo Serikali imeweka bei elekezi kwa  bidhaa muhimu za vyakula vinavyotumika zaidi katika Mwezi wa  Ramadhani.

“Ni matumaini yangu kwamba wafanyabishara wataitumia vizuri fursa hii  na watahakikisha malengo ya Serikali ya kuwapa wananchi  unafuu wa bei za bidhaa yanafikiwa, alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Mwezi wa Ramadhani umepewa hadhi na utukufu mkubwa na yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu kwani ni mwezi ambao imeteremshwa Qur-ani ambapi pia, ndani ya mwezi huu imeamrishwa kufunga.

“Tunamuomba  Mwenyezi Mungu atuwezeshe kutekeleza ibada ya saumu  vizuri na atunufaishe na neema zote  zilizoambatana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani”, alisema Rais Dk. Mwinyi. 

Rais Dk. Mwinyi aliwataka Waumini kuhakikisha sadaka wanazozitoa zinawafika  wanaostahili na wanaozihitaji zaidi kwani ni jambo la faraja kuona kwamba hivi sasa hapa Zanzibar zipo asasi nyingi za kiraia ambazo zinashughulikia ukusanyaji, upokeaji na ugawaji zaka na sadaka kwa wanaostahili na kurahisisha kuwatambua na kuwafika wenye kutoa pamoja na wale wenye sifa ya kupewa.

Alitoa nasaha kwa viongozi wa asasi zote zinazoshughulikia ukusanyaji na ugawaji wa zaka na sadaka zitekeleze wajibu wao kwa misingi ya  upendo na uadilifu kwani wakifanya hivyo watajenga imani na kuwapa nguvu zaidi wale wanaotoa  mali zao kwa lengo la  kutekeleza ibada hizo na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ibada ya funga, kwa hakika ina mafundisho mengi ikiwa ni pamoja na kufundisha kuishi kwa pamoja, kupendana na kusaidiana.

Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ibada ya funga inafundisha kuwa  wastahamilivu na wavumilivu, wenye subira na uwezo wa kuyadhibiti matamanio ya nafsi kwani funga ni fundisho na  kigezo cha subira, jambo ambalo ni muhimu katika maisha ya mwanaadamu na  limehimizwa na Mwenyezi Mungu katika aya mbali mbali kwenye Qur- ani  Tukufu.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.