Habari za Punde

Wizara Kushirikiana na Sekta Binafsi Kujenga Uchumi wa Kidikitali.

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akizungumza katika kikao na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika Mei 23, jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amefanya kikao na Wakandarasi wajenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano leo Mei 23 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Wizara anayoisimamia ipo tayari kujenga uchumi wa kidijitali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia inaamini katika ushirikiano na Sekta Binafsi katika kuendesha shughuli zake kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi akitolea mfano wa nchi jirani ya Kenya ambayo takwimu zinaonesha sehemu kubwa ya Mkongo wa Mawasiliano umejengwa na Sekta Binafsi kuliko uliojengwa na Serikali ambapo imesaidia ufikishaji wa huduma za mawasiliano kuwafikia watu wengi zaidi

“Inawezekana hapa na pale Sekta Binafsi imekutana na mawimbi mbalimbali lakini tunawahakikishia kuwa mawimbi yametulia na tupo tayari kufanya kazi pamoja na tuwahakikishie kuwa tutawalinda ili mradi mtimize wajibu wenu na mfanye kazi kwa kuzingatia muda, viwango na ubora wa kimataifa”, amezungumza Waziri Nape

Waziri Nape amesema kuwa wakandarasi wazawa wanafanya vizuri na ni matamanio ya Serikali idadi yao izidi kuongezeka ambapo amesema kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, 2022 jumla ya Mikataba 22 ya ujenzi wa kilomita 4,442 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano imeingiwa baina ya Wizara na Wakandarasi 8 ambao kati yao wakandarasi 6 ni wazawa na wakandarasi 2 wanatoka katika kampuni za nje zilizosajiliwa nchini

“Niliwaambia watendaji wa Wizara ninayoisimamia kuwa kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake, kwetu sisi hata wakandarasi ni zawadi ya Mungu kwa Wizara yetu na ndo maana tupo hapa tunawapenda na tunawajali, tutahakikisha tunafanya kazi pamoja, uwepo wenu unachangia mafanikio yetu, nyie mnatuhitaji na sisi tunawahitaji

Ameongeza kuwa Wizara hiyo bado ina kazi kubwa ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, hivyo fursa za kuendelea kufanya kazi na wakandarasi hao bado zipo lakini kipimo cha kuendelea kufanya kazi na Wizara hiyo ni kukamilisha kazi kwa kiwango, ubora na muda uliopangwa

Aidha, Waziri Nape amezishukuru Sekta za umma kwa kushirikiana katika kuwafikishia huduma wananchi huku akitolea mfano wa mashirikiano baina ya Wizara hiyo na TANESCO pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa makubaliano ya kutumia miundominu ya reli na ya umeme kupitisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kusababisha kilomita nyingi zaidi za Mkongo kujengwa tofauti na mpango wa awali

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema Wizara hiyo chini ya uongozi wa Waziri Nape umewaleta pamoja viongozi,watendaji na wadau wa Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kikao hicho na wakandarasi wajenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taif awa Mawasiliano ambapo  kupitia kikao hicho wamepata maono na muelekeo wa Wizara katika kuboresha utoaji wa huduma na kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni muundombinu muhimu katika sekta ya mawasiliano na ujenzi wa uchumi wa nchi unaoelekea katika uchumi wa kidijitali na watendaji wa Wizara hiyo wanalo jukumu la kuhakikisha nchi inafikia kwenye uchumi wa kidijitali

Katika hatua nyingine Waziri Nape ametoa cheti kwa kampuni Raddy Fiber Solution Ltd kwa kumaliza ujenzi wa Kilomita 72 Mangaka-Mtambaswala, Kilomita 265 Manyoni-Kambikatoto na ukarabati wa Mkongo wa Taifa Kilomita 105 Arusha-Namanga, Telecom Associates Ltd Kilomita 57 Bwanga-Chato) na Huawei kwa Upanuzi wa vituo 14 vya Mkongo

Kwa upande wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepewa cheti kwa kumaliza  ujenzi wa Kilomita 72 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliojengwa kuunganisha Ofisi za Serikali Dodoma pamoja cheti na nyaraka za michoro inayoonyesha jinsi na namna miundombinu ya Mkongo wa Taifa ulivyojengwa kutoka Mangaka-Mtambaswala (kilomita 72) na Arusha-Namanga (kilomita 105) ili kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha Mkongo huo. 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akimkabidhi cheti cha cha kukamilisha ujenzi wa kilomita 72 za  Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kuunganisha Ofisi za Serikali zilizopo eneo la Mtumba jijini Dodoma kwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Petter Ulanga katika kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye(Mb) akimkabidhi cheti na nyaraka za michoro Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga inayoonyesha jinsi na namna miundombinu ya Mkongo wa Taifa ulivyojengwa kutoka Mangaka-Mtambaswala (kilomita 72) na Arusha-Namanga (kilomita 105) ili kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha Mkongo huo.

  Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akimkabidhi cheti cha mradi wa Mkongo wa Taifa uliokamilika mwaka 2021/2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Kandarasi ya Raddy Fibre Solution Ltd, Ramadhani Mlanzi katika kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakifurahi na kupongezana na  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi mara baada kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (wa katikati aliyeketi) akiwa katika picha ya Pamoja na Wakandarasi wa Mkongo wa Taifa uliokamilika mwaka 2021/2022 mara baada ya Waziri Nape kuzungumza na Wakandarasi hao kwenye kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika  Mei 23, jijini Dodoma.

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.