Na Mwandishi wa GCLA
Maafisa Elimu Sekondari na Wakuu wa Shule za Sekondari
nchini wamesisitizwa kusimamia vyema maabara za kemia na kemikali na
kuhakikisha maabara hizo zinakidhi vigezo ambavyo sheria inataka.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkemia Mkuu wa
Serikali, Sabanitho Mtega wakati akifungua kikao cha Maafisa Elimu Sekondari na
Wakuu wa Shule za Sekondari wa mkoa wa Dar es Salaam kilichoandaliwa na Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na kufanyika mwishoni mwa wiki katika
ukumbi wa Hazina Jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kikao hiki, naamini mtaenda
kuyatekeleza yote yaliyojadiliwa hapa pamoja na kuibua changamoto ambazo
zitajitokeza lakini pia kuangalia namna bora ya kukabiliana nazo,” alieleza Mtega.
Aidha, Mtega aliwashauri wataalamu, walimu na
wanafunzi wanaotumia maabara za kemia na kemikali kufanya kazi kwa kutumia
vifaa maalum vilivyoainishwa ili kuhakikisha wanalinda afya zao na afya ya
jamii pamoja na kufuata sheria na kanuni za matumizi salama ya kemikali.
“Unapotumia kemikali unapaswa kufahamu aina za
kemikali na madhara yake kwa sababu kemikali nyingine zina madhara makubwa kwa
afya ya binadamu na mazingira na nyingine zimefutwa kutokana na Mikataba ya Kimataifa”.
alisisitiza Mtega.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Kenton ya Jijini
Dar es Salaam, Abdullah Kashogi aliipongeza Mamlaka kwa kutoa mafunzo hayo yenye
maelekezo muhimu ya kuzingatia matumizi
sahihi na salama ya maabara za shuleni.
“Semina hii imetupatia faida kubwa kwa sababu
shule nyingi za Sekondari zina maabara ambazo zinatumiwa na walimu na wanafunzi
hivyo maelekezo yaliyotolewa na wataalamu wa GCLA yametupa faraja na upeo wa
kuweza kujua kwamba wanafunzi wetu na walimu wao wanaweza kujilinda vipi na
madhara ya kemikali wakiwa maabara.” Alisema Kashogi.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA)
ina utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wanaotumia kemikali wakiwemo
wanafunzi ili kuhakikisha Mamlaka hiyo inatimiza matakwa ya kisheria ya kulinda
afya za watu na mazingira.
No comments:
Post a Comment