Habari za Punde

MKUTANO WA WATENDAJI WA AFYA KUHUSU AFYA YA UZAZI, MAMA NA MTOTO

Mwakilishi kutoka UNFPA  Zanzibar Dkt.Aza Said Amin akitoa maelezo kuhusu huduma ya mama na mtoto pamoja na afya ya Uzazi wakati wa mkutano maalum wa watendaji wa kada mbalimbali za Afya uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Ali Said Nyanga akizungumza na watendaji wa kada mbalimbali za Afya wakati akifungua mkutano maalum wa watendaji hao unaohusiana na tathmini ya Elimu ya Afya ya Uzazi huko Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.
Afisa Takwimu na ufatiliaji kitengo shirikishi cha Afya ya Uzazi na Mtoto akiwasilisha ripoti ya miezi sita kuhusiana na Afya ya mama na mtoto huko Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Ali Said Nyanga akizungumza na watendaji wa kada mbalimbali za Afya wakati akifungua mkutano maalum wa watendaji hao unaohusiana na tathmini ya Elimu ya Afya ya Uzazi huko Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.

Na.Rahima Mohamed - Maelezo Zanzibar.  29/06/2022

Wizara ya Afya  imeamua  kuchukuwa hatua madhubuti  na kuhakikisha wanaondosha changamoto zinazowakabili ili kupunguza  vifo vya mama na mtoto nchini.

 

Hayo amesema Mkurugenzi wa Kinga na elimu ya afya Dr. Ali Said Nyanga wakati akifungua mkutano wa mwaka wa kujadili afya ya mama na mtoto huko ukumbi wa chuo cha utalii Marughubi Mjini Zanzibar.

 

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inajenga hospitali za Wilaya na  kuongeza sehemu za kujifungulia ili kuondosha msongamano wa kwenda kujufungulia Hospitali ya Mnazimmoja kwa lengo kupunguza vifo vya mama na mtoto.

 

Amesema lengo la mkutano huo ni kujifunza mambo mbalimbali na kuandaa mikakati madhubuti itakayoongeza hamasa ya utendaji kazi  pamoja na kuzuia uzembe ambao utapelekea vifo kwa mama wanapofika kujifungua hospitalini.

 

Aidha amesema Wizara ya afya inathamini juhudi zinazotolewa na mashirika ya afya kwa kusaidia  kupitia nyanja mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.

 

Vilevile amewataka watendaji wabadilike katika kutoa huduma kwa  kuongeza usimamizi na ukaguzi katika vituo vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.

  

Nae kaimu meneja kitengo Shirikishi Afya ya mama na mtoto Dkt Farhat Jowhar Khalid amesema mkutano huo ni muhimu sana na utasaidia kutafuta njia mbadala ili kuzidhibiti vifo na kuboresha huduma ya mama na mtoto nchini.

 

Nae muwakilishi kutoka shirika la UNFPA Dkt Azza Said Amiin amesema Shirika lake linaunga mkono juhudi za serikali za kupunguza vifo vya mama na mtoto  kwa kuimarisha upatikanaji wa dawa,vifaa tiba pamoja na kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa wafanyakazi ili kutoa huduma bora za afya ya uzazi.

 

Aidha ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimarisha sekta ya afya na kuweka mazingira mazuri kwa mashirika ya umoja wa Mataifa na washirika wengine wa maendeleo yanayounga mkono juhudi za kuokoa vifo vya mama na mtoto .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.