Habari za Punde

Sauti ya Wajane Kuazia Mashinani : WAZIRI DKT. GWAJIMA

Na MJJWM, Dodoma.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Dorothy Gwajima amesema kuelekea Siku ya Wajane Duniani 2022 maadhimisho yatafanyika ngazi ya chini kwenye mitaa ikiwa ni mwanzo wa kuadhimisha siku hiyo Kitaifa kwa miaka mingine ijayo.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wajane kupitia Vyombo vya Habari Juni 22, 2022 jijini Dodoma.

Waziri Gwajima alisema Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuwasaidia Wajane nchini kuondokana na kero  kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo baada ya kufiwa na wenza wao.

“Tunatambua kwamba Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ni jukwaa linalowaleta pamoja wajane na kuwapa  fursa ya kushiriki na  kubaini changamoto wanazokumbana nazo na hata kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. Vilevile “ alisema Dkt Gwajima.

Ameongeza kuwa, kwa Tanzania huadhimisha Siku ya Wajane kwa lengo la kukuza hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya jamii ili kuacha ukiukaji wa haki za binadamu kwa wajane. Hivyo, kama Taifa, maadhimisho haya yanatoa fursa ya pamoja katika kubaini changamoto za wajane na namna ya kukabiliana nazo .

Kwa upande wake Mratibu wa Wajane Tanzania Bi Mariamu Aswile  alikemea vikali vitendo vya  unyanyaswaji kwa Wajane  na kuiomba Serikali kufanya marekebisho kwenye Sheria zinazohusu Mirathi.

“Sheria za mirathi zipitiwe upya kwani wajane wanapitia wakati mgumu sana katika kudai haki zao  maana huchukua  muda mrefu mpaka kufikia wakati wanapoweza kupata haki zao hivyo kujikuta wanapoteza muelekeo wa ndoto zao” amesemea Mariam.

Naye mmoja wa wajane Bi. Christina Njavike aliiomba Serikali kutoa elimu kwa Wajane kuhusu namna ya kupata haki zao kwani kujua haki kwa Wajane kunaepusha wanawake kunyanyaswa na ndugu wa wenza wao wenye nia mbaya.

“Sipendi tukae kinyonge  eti kisa ni Wajane, tukipata fursa za kufanya kazi basi tufanye kweli Sheria zipo  Wanawake tusiwe waoga tupambanie haki zetu na inapotokea mtu amenyanyaswa tusaidiane” amesisitiza Bi Njavike.

Siku ya Wajane Duniani huadhimishwa kila mwaka Juni, 23 na kwa mwaka huu Siku hii inaongozwa na Kaulimbiu isemayo "Utu  Uwezeshaji wa Kiuchumi na Haki za Kijamii kwa Wajane"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.