Habari za Punde

Wadau wa kilimo watakiwa kuungana kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Nane la Mwaka la Sera kwa Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakiwa katika Kongamano la Nane la Mwaka la Sera kwa Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi jijini Dodoma 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (wa tatu kushoto) akiwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira na kilimo mara baada ya kushiriki Kongamano la Nane la Mwaka la Sera kwa Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi jijini Dodoma Juni 6, 2022.

(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Wadau wa kilimo wametakiwa kuungana kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kulinda na kuhifadhi misitu, vyanzo vya maji na rasilimali zote tegemeo la kiuchumi na kijamii.

Wito huo umetolewa Juni 6, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akishiriki kwenye Ufunguzi wa Kongamano la Nane la Mwaka la Sera kwa Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa misitu ndani Mashariki na Kusini mwa Afrika ambako takribani hekta milioni 48.1 ni eneo la misitu lakini pamoja na hayo takribani hekta 469,420 hupotea kila mwaka kwa sababu ya shughuli za kilimo, makazi, shughuli nyingine za kijamii.

Khamis aliwaomba wataalamu kuona nanma ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi hasa kuni na mkaa kwa kuhamasisha matumizi ya majiko ya kupikia yanayotumia nishati vizuri na mkaa wa kisasa.

“Niwaombe wadau wetu wa kilimo, mifugo na uvuvi muangalie teknolojia, mbegu, afya ya udongo, mbolea  na viuatilifu ambavyo kwenye sekta hii vinaweza kusaidia sana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Khamis.

Alisema sehemu nyingi hapa nchini ambazo zilikuwa zina misitu na uoto wa asili, zilikuwa zinapata mvua mara mbili hadi tatu kwa mwaka na sasa hivi zinapata mara moja na pengine hakuna kabisa na hivyo shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi katika maeneo hayo zimeathirika.

Hivyo, alisema upotevu huu wa miti husababisha pia ongezeko la hewa ya ukaa ambayo huchangia kuongezeka kwa joto ambapo inakadiriwa kuwa hadi mwaka 2080, joto hapa nchini litakuwa limeongezeka kati ya nyuzi joto 1.40C hadi 3.60C na kupungua kwa mvua hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi zikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi. 

Naibu Waziri Khamis alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imejipanga kuhakikisha Sera, Sheria, miongozo na Mikakati mbalimbali ya Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinafanyiwa kazi.
Kongamano hilo la siku tatu  linalowashiriki wadau mbalimbali kutoka sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazingira lina Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya mazao, mifugo, uvuvi na mazingira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.