Habari za Punde

Waziri Mchengerwa: Kiswahili Ndiyo Silaha Yetu


Na. Eleuteri Mangi-WUSM, Dodoma

Lugha ya Kiswahili ni silaha ya taifa letu, imekuwa ya kwanza kutoka Bara la Afrika kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambayo inawazungumzaji wazungumzaji wengi zaidi ya milioni 200 duniani kote.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo Juni 6, 2022 wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

“Ni kwa kutambua umuhimu wa johari hii ya thamani na furaha yetu kwa mafanikio haya, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara hii inaendelea na mikakati ya kuiongoza dunia kuadhimisha Siku hii kwa mara ya kwanza Julai 7, 2022 katika Balozi zetu kote Duniani, kama wasemavyo Waswahili “Hamadi ni ilio kibindoni, na silaha ni iliyo mkononi” Kiswahili ndiyo silaha yetu” amesema Waziri Mchengerwa.

Lugha adhimu ya Kiswahili imeendelea kukua na kuimarika na kukubalika kutumika kitaifa, kikanda na kimataifa hatua inayolitangaza vema taifa duniani.

“Naweza kujinasibu kuwa matumizi ya Kiswahili yanazidi kukubalika kitaifa, kikanda na kimataifa ambapo jitihada hizo kwa kipindi cha mwaka 2021/22 zimezaa matunda kwa Kiswahili kuvishwa joho jipya kuwa lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika” amesema Waziri Mchengerwa.

Pia ameliambia Bunge kuwa Kiswahili kimepitishwa kuwa lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Februari 5 - 6, 2022 Jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango.

Waziri Mchengerwa amesema kuwa hatua hiyo ni fursa muhimu kwa Wataalamu wa Tafsiri na Ukalimani nchini ambao katika muda mfupi, tayari Watanzania 65 wamesajiliwa kupata fursa za ajira za muda na za kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni zake.

Aidha, Kiswahili, kuendelea kushamiri, baadhi ya Vyuo Vikuu vya nje ya Tanzania ambavyo awali havikuwa na programu za Kiswahili vimeanza kuingiza Kiswahili katika programu zao ambapo tayari kuna makubaliano ya awali ya kushirikiana kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ethiopia, Chuo Kikuu cha Port Harcourt (Nigeria) na Chuo Kikuu cha Joachim Chisano (Msumbiji) katika kufundisha Kiswahili.

Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa juhudi za Serikali pamoja na wadau wa Kiswahili zimewezesha lugha hiyo kupitishwa na rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23, 2021 na kupewa siku yake maalum ambapo Julai 7 ya kila mwaka imetambuliwa na kupewa heshima ya kuwa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani. 

Msingi wa uamuzi huo unatokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika kukiasisi na kukiendeleza Kiswahili ambayo ni historia adhimu ya taifa letu ambapo Julai 7, 1954 Mkutano Mkuu wa TANU chini ya Uenyekiti wa Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, uliamua kwa kauli moja kutumia Kiswahili kwa lengo la kuleta umoja kwa Watanganyika wote katika harakati zao za ukombozi.

“Uamuzi huu ni wa kihistoria; kwani kwa mafanikio haya Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Kiafrika ambayo imepangiwa siku maalumu ya kusherehekewa na kuadhimishwa Kimataifa, “Chanda chema huvishwa pete” amesema Waziri Mchengerwa.

Ili kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kukua na kuenea duniani, Serikali kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo lipo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo limekuwa kinara wa kueneza lugha hiyo duniani.

Dunia ilishuhudia kupitia vyombo vya habari vya ndani nan je ya nchi kuanzia Machi 14–18, 2022 ambapo Serikali iliandaa Kongamano la Waandishi na Watangazaji wa Idhaa za Kiswahili Duniani lililofanyika Jijini Arusha na kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Philip Isdor Mpango na kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambapo washiriki takribani 250 kutoka redio na televisheni za ndani na nje ya nchi walishiriki na litaendelea kufanyika kila mwaka.

Hatua hiyo inaendelea kuliweka taifa la Tanzania ambalo ipo katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye ramani ya dunia na kutambuliwa na shirika la UNESCO kuwa ndiyo ndiyo chimbuko la lugha adhimu na aushi ya Kiswahili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.