Habari za Punde

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi ameipongeza benki ya CRDB kwa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo wakiwemo wajasiriamali.

Akizungumza mara baada ya kufungua tawi la benki ya CRDB Wete Pemba Dk, Mwinyi alisema kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa wananchi, ambayo inasaidia kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

Alieleza kuwa, benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo endelevu na ndio maana imekuwa ikitoa misaada kwa ajili ya kukuza vipato vya wananchi.

"Tuliwaomba wafungue Tawi jengine kwa Pemba na tunashukuru kwa kutimiza ahadi hii, hii ni kuonyesha wazi ushirikiano mkubwa walionao kwa Serikali yetu", alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa kipindi cha kampeni aliahidi kuwapatia nyenzo wajasiriamali na kusema kuwa atahakikisha anatimiza ahadi hizo kwa vitendo.

"Hapa leo ninawakabidhi mikopo ya boda boda na pia wakati tukiendelea na ziara hii tutawapatia wajasiriamali fedha na vifaa mbali mbali vitakavyowasaidia katika utendaji wa kazi zao ", alifafanua Rais Dk. Mwinyi.

Akiweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Kinyasini Wete Dk, Mwinyi alieleza kuwa lengo la Serikali ni kuwafikishia huduma bora za afya wananchi wake.

Alisema kuwa, huduma hiyo ya hospitali ya Wilaya itasaidia kuondosha changamoto ya wananchi kuifuata huduma hiyo masafa marefu, ambapo zamani walikuwa wanakwenda katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani na hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

"Hospitali hii ya kisasa itakuwa na vifaa vya kisasa na kutoa huduma bora sambamba na kuongeza wafanyakazi wa afya wakiwemo madaktari", alisema.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka wafanyabiashara na wananchi kudai risiti ya elektroniki wakati wanaponunua bidhaa, ili kuongeza mapato ambayo husaidia Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Abdul-Majid Nsekela aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa utendaji wao wa kazi nzuri wa kuwatumikia wananchi na kuhakikisha wanakuwa na Maendeleo ya kiuchumu.

Alisema kuwa, wanajivunia sana kuona Serikali inakuwa sehemu ya mafanikio yao kwani imekuwa ikishiriki kikamilifu katika shughuli zao za kuwapatia wananchi maendeleo.

"Tunaendelea kutoa huduma mbali mbali kwa wananchi na kwa sasa tuna matawi na pia tumewaongezea huduma za mawakala", alieleza Mkurugenzi huyo.

Alifafanua kuwa, tayari wameshaviwezesha vikundi 607 vikiwa na watu 11,806 ambao wamechukua mkopo wenye thamani ya TZS bilioni 6.7 katika benki hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum alisema, sekta ya benki imekuwa ikichangia uchumi wa Zanzibar kwa asilimia 3.4 kwa mwaka, hivyo kuna haja ya kuwapongeza kutokana na kodi inayopatikana katika benki hizo.

"Tunajitahidi kuona kwamba miradi yote inakwenda vizuri na kuhakikisha fedha zote zinazotoka zinaingizwa kwenye miradi yote, hatutokuwa tayari kukwamisha utekelezaji", alisema Waziri huyo.

Wakati huo huo, Rais Dk, Mwinyi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Skuli ya ghorofa ya Jadida Wete alikipongeza Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar, KMKM kwa juhudi zake za kuhakikisha majengo wanayojenga yako katika viwango vizuri.

Alisema kuwa ujenzi atahakikisha unamalizika kwani Mkoa wa Kaskazini Pemba umeweza kufanya vyema kwenye matokeo ya mitihani yao ya kitaifa licha ya changamoto mbali mbali walizonazo ikiwemo uhaba wa Walimu na msongamano wa wanafunzi madarasani.

Dk, Mwinyi alieleza kuwa itakapo malizika Skuli hiyo na kutowa nafasi kwa wanafunzi kuondokana na msongamano anaimani kubwa matokeo mazuri zaidi yatapatikana.

“Nina imani tukimaliza ujenzi huu na wanafunzi wakipata nafasi kubwa ya kukaa madarasani basi ni wazi watafanya vizuri zaidi kama walivyofanya mara hii kwani tayari Serikali inampango wa kuajiri walimu wa ziada ili waweze kusaidiana na walimu waliopo”, alisema Rais Dk. Mwinyi.

Akijibu maombi ya wananchi wa Jimbo la Wete kuhusu ujenzi wa barabara, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mpango wa kuzijenga barabara za ndani uko pale pale na kwamba sasa zitajengwa kwa kiwango cha lami badala ya kifusi.

Dk, Mwinyi alieleza kuwa ataiagiza Wizara ya Afya kuifanyia matengenezo Hospitali yao ya Jadida ili iweze kurejea katika hali yake na kutowa huduma kwa  wananchi wa maeneo hayo.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa bandari ya Wete, alisema kuwa Serikali iko mbioni kuifanyia matengenezo bandari hiyo ili iweze kutowa ajira kwa wananchi ikiwemo Vijana na juhudi mbali mbali za ujenzi huo tayari zimeshaanza kufanyika.

Ziara hiyo ya siku moja kwa Wilaya ya Wete ina lengo la kukagua, kufungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ikiwemo ya UVIKO- 19.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.