Habari za Punde

Alhaj Dk. Hussein Amewapongeza Waumini wa Masjid Nabawi Mbuyu Mnene Kwa Kushiriki Masuala ya Kijamii

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Masjid Nabawi Mbuyu Mnene Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid hiyo leo 26-8-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewapongeza waumini wa Msikiti wa  ‘Masjid Nabawi’ ulioko maeneo ya Mbuyu Mnene, Mkoa Mjini Magharibi kwa kuwa mfano mwema katika kushiriki masuala mbali mbali ya kijamii.

Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo katika salamu zake kwa waislamu wa msikiti huo baada ya kukamilisha   Ibada ya sala ya Ijumaa.

Amesema waumini wa msikiti huo wamekuwa wa kwanza kutekeleza kwa vitendo yale aliyokuwa akiyabuhiri katika msikiti mbali mbali, juu ya umuhimu wa waislamu kushikiri katika masuala ya kijamii, kama vile kusaidia Mayatima, wajane, walemavu, wenye mahitaji pamoja na kusimamia usalama wa maeneo yao.

Alisema hatua ya waumini wa Msikiti huo kutoa hundi ya shilingi 500, 000 kwa serikali ili kusaidia huduma nyengine za maendeleo au kijamii, ni za kupongezwa na mfano mwema.

Alielezea kuwa mchango huo aliokabidhiwa na uongozi wa msikiti huo sio mdogo na kusema utasaidia maeneo mengine yenye mahitaji.

Aidha, aliwataka wananchi kote nchini kuwa na subira wakati huu wakisubiri makarani wa sensa wapite katika maeneo yao na kukamilisha zoezi la kuhesabu watu ili Serikali iweze kupanga mipango yake maendeleo.

Nae, Katibu Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema sensa ni sunna kwa sababu Mtume Muhammad (SAW)  yeye mwenyewe alifanya sensa kwa kutaka kutambua idadi ya watu walioingia katika Dini hiyo, hivyo akatoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki katika zoezi hilo linaloendelea kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mapema, Imamu wa Msikiti huo Sheikh Ali Aboud alisema msikiti huo umekuwa kiunganishi kikubwa cha watu na kubainisha namna wananchi wanavyoishi vyema kama ndugu pamoja na kushirikiana katika masuala mbali mbali, yakiwemo ya kijamii.

Alitoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj  Dk. Hussein Mwinyi  kwa kufika msikitini hapo na kuswali pamoja na waumini wa msikiti huo, ambapo kw amuda mrefu walisubiri jambo hilo.

Aidha, Khatibu katika sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Suleiman aliwataka waislamu kuzingatia wakati ili kufikia malengo yao katika maendeleo ya dunia na akhera.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.