Habari za Punde

DC Moyo : Atakayepotosha Kuhusu Chanjo ya Uviko-19 Kuchukuliwa Hatua za Kisheria

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na wananchi juu ya umuhimu wa kupata chanjo ya UVIKO 19
Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akigawa kadi kwa ajili ya wananchi wanaoendelea kupata chanjo ya UVIKO 19
Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akishudia daktari akiwa anawachanja wananchi chanjo ya UVIKO 19.

Na Fredy Mgunda, Iringa.

MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amesema kuwa watu wote wanaopotosha kuhusu zoezi la chanjo ya UVIKO 19 watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kupotosha jamii.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Ifunda na Maboga mkuu wa wilaya ya Iringa alisema kuwa chanjo ambavyo inatolewa kwa wananchi haina madhara yoyote yale bali inasaidia kuwaongezea kinga ya mwili ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Moyo alisema kuwa hakuna serikali yoyote ile ambayo inataka kuwauwa wananchi kwa kuwapatika chanjo yenye madhara bali serikali inajukumu la kuwalinda wananchi kwa gharama yoyote.

Alisema kuwa baada ya maneno ya uongo na dhana potofu kuonekana kuwa ni propaganda zisizo na maana yoyote, wananchi wameamua kushiriki chanjo ya UVIKO-19 kwa manufaa yao.

“Mara nyingi kitu kigeni kikitokea kuna baadhi ya watu wanapotosha na kuzungumza ndivyo sivyo juu ya jambo hilo utadhani wanalitambua kumbe hawafahamu ila hili la UVIKO-19 wengi wao wamelitambua na kulielewa ndiyo sababu wamejitokeza kwa wingi kuchanja,” anasema Moyo

Alisema kuwa zoezi la chanjo ya UVIKO 19 inaendelea vizuri wilaya ya Iringa na zaidi ya wananchi 48,434 wamefanikiwa kuchanja chanjo ya UVIKO 19 kwa lengo la kuendelea kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Colona ambao umeshasababisha vifo vingi vya wananchi wa wilaya hiyo.

Moyo alisema kuwa hadi kufikia tarehe 26/7/2022 walikuwa wamewafikia jumla ya wananchi 48,434 ambao wamepata chanjo ya UVIKO 19 dozi ya pili ya chanjo ya Janssen ambayo ni sawa na asilimia 39.24 ya walengwa 123,418.

Moyo alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wananchi waliokuwa na miaka 18 na kuendelea waweze kupata chanjo ya UVIKO 19 katika kipindi cha kampeni ndogo inayoendelea hivi sasa katika wilaya ya Iringa.

Alisema kuwa kwa sasa wilaya ya Iringa imetenge jumla ya vituo 79 vinavyotoa huduma za chanjo pamoja na zoezi la uchanjaji katika vituo watoa huduma wanaotumia huduma za mkoba ili kuwafikia wananchi popote walipo.

Moyo alisema kuwa viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali kama shule,vyuo, viongozi wa bajaji, daladala,bodaboda,saluni,vikoba, viongozi wa dini,siasa wadau wa afya,wazee mashuhuri na wazee wa kimila kuhakikisha wanashirikiana na serikali ya wilaya ya Iringa kuhamasisha jamii ili iweze kupata chanjo ya UVIKO 19.

Alisema kuwa wataalamu wa afya na jamii wanapaswa kupongezwa kwa namna ambavyo wamekuwa wanalishughulikia suala la kitaifa kwa kuwa inaonyesha kwa namna gani wanavyojitoa kutoa elimu kwa wananchi hadi wanachanja kwa hiyari chanjo ya UVIKO 19.

Moyo alisema kuwa anatarajia wananchi ambao hawajapata chanjo ya UVIKO-19 watashiriki kupata chanjo hiyo ambayo inaendelea kutolewa na wataalamu wa afya.

“Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwaasa wananchi kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani maradhi hayo bado yapo nchini hivyo tushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19,” amesema

Mkazi wa kata ya Ifunda Winfrida Mwinuka anasema wataalamu wa afya wamekuwa wanafika hadi vijijini na kutoa elimu kwa jamii kIsha kuwapatia chanjo hiyo ya UVIKO-19.

“Hadi hivi sasa elimu inaendelea kutolewa kwa jamii huku vijijini na wanaitikia ushauri wa kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 kwani wanatambua kuwa ukipata maradhi hayo bila kuchanja utapata matatizo makubwa kwenye changamoto ya kupumua pindi ukiupata ugonjwa huo,” anasema.

Mkazi wa kijiji cha Kipongero Majaliwa Lalika anasema kuwa viongozi na wananchi wa Wilaya ya Iringa kwa pamoja wameungana katika kuhakikisha wanapata chanjo ya UVIKO-19 ndiyo sababu ya wananchi kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO 19.

“Mtu anaona atapata maambukizi ya UVIKO-19 yeye mwenyewe na hayo ni maradhi ambayo hayana matibabu hivyo ameona hawezi kupata tatizo kisa kutochanjwa kwa kutosikiliza wataalamu wa afya na kuwasilikiza wazushaji,” anaeleza

Hivi karibuni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza hivi karibuni kwenye tamasha la MZIKI MNENE lililofanyika uwanja wa Nangwanda Mkoani Mtwara amesema imethibitika kuwa njia ambayo ni salama ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 ni kupata chanjo kwani ukichanja utakuwa umejikinga na kuikinga jamii ya watanzania.

Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea kuwalinda wananchi wake katika maambuzi ya magonjwa mbalimbali kwa kutoa chanjo ikiwemo ya UVIKO-19.

“Sisi kama Wizara ya Afya tutatumia mbinu mbalimbali ambazo zitakazowafikia wananchi kama tunavyotumia matamasha haya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupata huduma ya chanjo ya UVIKO-19,” anamaliza kwa kusema Waziri Ummy.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.