Habari za Punde

Mhe.ULEGA: Vijana Changamkieni Fursa za Uchumi wa Buluu

Na Mbaraka Kambona, Mwanza

 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza vijana wa Kanda ya Ziwa Viktoria kufuga samaki ili kujiongezea kipato na kuongeza fursa za ajira nchini.

 Waziri Ulega alitoa wito huo kwa nyakati tofauti akiwa ziarani katika Wilaya za Ukerewe na Ilemela zilizopo mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki.

 Alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kutumia fursa za uchumi wa buluu zilizopo ndani ya Ziwa Viktoria kuwawezesha vijana kufuga samaki kwa kutumia vizimba na kuuza samaki hao ndani na nje ya nchi ili kujiongezea kipato.

 "Rais Samia ametoa bilioni 20 kwa ajili ya kuwezesha vijana kufuga samaki katika vizimba, hivyo ni wakati sasa wa kujipanga ili pesa hizo zitakapokuja tuweze kuzitumia vizuri kufanya uzalishaji wa samaki kwa wingi ili tuweze kuuza na kupata kipato", alisema

 Aliongeza kwa kusema kuwa samaki aina ya sato wanahitajika sana ndani na nje ya nchi, uhitaji ni mkubwa hivyo vijana wajipange vizuri ili waweze kutumia fursa hiyo kujiinua kimaisha.

 Kwa upande wa vijana wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki, Bw. Bahati Paul kutoka Ilemela na Peter Emmanuel kutoka Ukerewe kwa nyakati tofauti walisema kuwa mpango huo wa Serikali wa kuwawezesha vijana utasaidia sana vijana kujiajiri na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

 Aidha, vijana hao waliiomba Serikali kutatua changamoto ya chakula cha samaki kwani imekuwa ikichangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa samaki nchini.

 Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alisema mwaka huu pia Serikali itawakopesha wavuvi nchini kote boti za kisasa zaidi ya 150 ili wavuvi waweze kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa samaki.

 Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitafungamanishwa na teknolojia za kisasa zitakazomsaidia mvuvi kurahisisha shughuli za uvuvi.

 Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa mkopo huo wa masharti nafuu unalenga kuwawezesha wavuvi kuboresha uvuvi wao kwa sababu nia ya  Mhe. Rais Samia ni kuwatoa wavuvi katika uvuvi wa kuwinda na kufanya uvuvi wa kisasa wa uhakika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.