Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiwasilisha hoja ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022,
bungeni jijini Dodoma.
Na Farida Ramadhani na Saidina Msangi WFM - Dodoma.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa mwaka 2022 (The Written Laws (Financial Provisions) Amendment Act, 2022), ambao unalenga kufanya marekebisho ya Sheria 6 za kodi, mirahaba na uwekezaji.
Akiwasilisha Muswaha huo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema Lengo la Muswada huu ni kufanya marekebisho kwenye Sheria zinazosimamia kodi na mrabaha kwa kubadili viwango vya kodi na mrabaha.
Aliongeza kuwa Muswada huo unalenga kuweka taratibu za utoaji vivutio kwa wawekezaji ili kuhamasisha uzalishaji kwa viwanda vya ndani ya nchi vinavyozalisha mbolea na maguni ya mkonge, pamoja na kuondoa changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria ya uwekezaji Tanzania, Sura 38.
Mhe. Nchemba alizitaja Sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia Muswada huo kuwa ni Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura 147, Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332, Sheria ya Madini Sura 123, Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura 220 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura 148.
“Sehemu ya Pili ya Muswada yenye ibara za 3 hadi 5 inapendekeza kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147, ambapo kifungu cha 128 kinapendekezwa kurekebishwa ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha, baada ya kupata idhini ya Baraza la Mawaziri kusamehe ushuru kwenye bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji mahiri na mahiri maalumu itakayoidhinishwa na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC)”, alifafanua Dkt. Nchemba.
Alibainisha kuwa iwapo itabainika kwamba msamaha uliotolewa kwa mwekezaji umetumika tofauti na malengo yaliyokusudiwa, msamaha husika utafutwa na mwekezaji atalazimika kulipa kodi iliyosamehewa.
“Marekebisho haya yanayopendekezwa yanalenga kuwianisha masharti ya Sheria hii na masharti ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania ili kuboresha utekelezaji wa vivutio vitakavyotolewa kwa wawekezaji”, alisema Mhe. Nchemba.
Alisema sehemu hii inapendekeza kurekebisha Jedwali la Nne la Sheria hii, kwa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo unaotokana na zao la zabibu unaoingizwa kutoka nje ya nchi kutoka shilingi 2,466.45 kwa lita hadi shilingi 5,600 kwa lita.
“Lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kuwezesha mvinyo unaozalishwa na zabibu zinazolimwa hapa nchini kuweza kushindana kwenye soko la ndani na mvinyo unaotoka nje ya nchi. Hali hii itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa soko la zabibu zinazolimwa nchini”, alisema Mhe. Nchemba.
Waziri Nchemba alisema Muswada huu pia unalenga kutoa unafuu wa gharama za malighafi kwa wazalishaji wa ndani wa bidhaa za mbolea na Serikali ina imani kwamba, unafuu huu unaotolewa kwa wazalishaji wa mbolea utaleta matokeo chanya kwenye upunguaji wa bei ya mbolea kwa wakulima, na hivyo kupunguza mzigo kwa Serikali katika utoaji fedha za ruzuku kwenye mbolea.
Alisema Muswada huo umefanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura ya 220, ili kumpa Waziri mamlaka ya kusamehe ushuru wa mafuta kwa miradi ya uwekezaji mahiri na mahiri maalumu itakayoidhinishwa na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji.
” Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya Sheria hii na masharti ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania ili kuwezesha utekelezaji wa vivutio vitakavyotolewa kwa wawekezaji”, alifafanua Mhe. Nchemba.
Alibainisha kuwa ili kuhakikisha kwamba, mafuta yanayopewa msamaha hayatatumika vibaya, Hati za msamaha wa kodi zitakazotolewa pamoja na mambo mengine zitabainisha muda wa kuanza na kumalizika kwa msamaha husika, kiwango cha mafuta kinachopewa msamaha pamoja na mradi unaonufaika wa msamaha.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaweka utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miradi husika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania na wadau wengine wa Serikali, ili kuhakikisha kwamba mafuta husika yanatumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema Muswada huo pia unalenga kuwianisha masharti ya Sheria hii na masharti ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania kuhusu utoaji wa vivutio vya kodi kwa wawekezaji.
Wakichangia muswada huo wabunge walipongeza muswada huo wakieleza kuwa utasaidia kuinua wakulima haasa wa zabibu kwa kuwa na uhakika wa soko na kusisitiza watakaopewa msamaha kutumia msamaha huo kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande akitetea jambo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. David Silinde, bungeni jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment