Habari za Punde

Idadi ya visiwa vinavyokodishwa Zanzibar yafikia kumi na saba (17) - Mhe Soraga

Na.Mwandisi ORKUU

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la pandani Mhe Prof. Omar Said Fakihi kuhusu maendeleo ya mchakato wa Serikali katika ukodishwaji wa visiwa vidogo vidogo kwa ajili ya Uwekezaji, katika kikao cha kumi na tatu cha Baraza kumi la Wawakilishi huko Chukwani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja

 

Amesema Serikali baada ya kuvikodisha Visiwa Kumi (10) vya mwanzo kwa ajili ya uwekezaji imeendelea na mchakato wa kutangaza visiwa vyengine 10 kwa Uwekezaji ambapo visiwa 7 kati ya hivyo vya Awamu ya Pili tayari wameshajitokeza wawekezaji na kufanya idadi ya Visiwa vyote vilivyokodishwa kufikia 17 hadi kufikia mwezi Septemba 2022.

 

Waziri Soraga amefahamisha kuwa awali Serikali ilikuwa ikiangalia zaidi mapato yatokonayo na kodi ya ukodishwaji wa ardhi (Land Lease) katika visiwa vinne vilivyokodishwa ambavyo ni Mnemba, Chapwani, Changuu na Bawe lakini sasa Serikali inatarajia kukusanya Dola za Kimarekani Milioni 19.8 kama malipo ya awali na Mtaji wa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 442.5 amabzo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Nchi na Wananchi wa Zanzibar

 

“Serikali haijasita kuvikodisha visiwa vyengine, bali Serikali inaendelea kuvitangaza visiwa ambavyo vina muonekano wa kuvutia wawekezaji kwa mujibu wa masharti yanayowekwa.”

 

Akielezea vigezo vilivyowekwa kupitia mamlaka ya Kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa wawekezaji wanaotaka kukodi visiwa hivyo amesema ni pamoja Uwezo wa mwekezaji katika kuhifadhi mazingira na kisiwa, uwezo wa kifedha, ushirikiano baina ya mwekezaji na jamii, aina ya uwekezaji unaotaka kufanyika pamoja na malipo ya awali ya ukodishwaji wa Visiwa ambapo hadi sasa malipo ya awali ya Dola za Kimarekani Milioni 11.1 yameshalipwa kwa baadhi ya Visiwa vilivyokamilisha vigezo hivyo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.