Habari za Punde

WAZIRI JAFO ATETA NA BALOZI WA SWEDEN

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na Balozi wa Sweden nchini Bi. Charlotta Ozaki Macias leo Septemba 2022 ofisini kwa Waziri jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweden nchini Bi. Charlotta Ozaki Macias pamoja na Ujumbe alioambatana nao mara baada ya kufanya kikao leo Septemba 2022 ofisini kwa Waziri jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Bi. Charlotta Ozaki Macias leo Septemba 2022 katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine mazungumzo yao yalihusisha ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Sweden katika utekelezaji wa miradi ya utunzaji na hifadhi ya mazingira.

Balozi Charlotta alielezea miradi ya matumizi ya nishati mbadala inayotekelezwa kwa ufadhili wa Sweden kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Aidha alielezea jinsi nchi hiyo ilivyojizatiti kushirikiana na mataifa ya Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hususan katika kushiriki Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika nchini Misri Novemba 2022.

Katika kikao hicho Balozi Charlotta aliambatana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Scania Tanzania Bi. Johanna Lind ambaye aliwasilisha mpango wao wa kuingiza malori aina ya Scania yanayotumia gesi (Compressed Natural Gas -CNG) na BIOGAS badala ya Diesel kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na uchafuzi wa mazingira.

Alisema matumizi ya gesi ni rahisi na nafuu zaidi kuliko dizeli huku akielezea changamoto iliyopo ni gharama zitokanazo na kodi na vituo vya kujazia gesi ambapo uwekezaji unahitajika.

Waziri Jafo alimshukuru balozi huyo kwa ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Sweden hususan kwa mchango wa nchi hiyo katika sekta mbalimbali za maendeleo ya Tanzania na kuahidi kuendeleza uhuaiano huo mzuri hasa katika eneo la Mazingira.

Pia, aliipongeza kampuni hiyo kwa kuja na mpango wa matumizi ya gesi katika magari yao na kuahidi kupata ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mpango huo na ikiwezekana uingizwe katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (DART).

Wengine walioambatana na Balozi ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Biashara (Ubalozini) Joakim Ladeborn na Bi. Eliavera Timoth (Meneja wa Kitengo cha Biashara - Scania).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.