MKUU wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba amewapongeza wananchi wa
kijiji cha Kizimkazi Mkunguni kwa
jitihada zao za kujitafutia maendeleo na
kukuza kipato chao kupitia sekta ya uvuvi.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pongezi hizo
huko Kizimkazi Mkunguni wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji
hicho katika hafla ya uzinduzi wa
uvunaji wa pweza ambapo wananchi hao walirimbika kwa muda wa miezi mitatu.
Alisema kuwa kusimamia urimbikaji wa
pweza unahitaji ujasiri mkubwa kwani
kuna baadhi ya wasio waaminifu huharibu kwa makusudi taratibu zinazowekwa na kuingia baharini kuiba pweza waliorimbikwa.
Hivyo, alitumia fursa hiyo kuwapongeza na
kuwashukuru wananchi wa kijiji cha kizimkazi Mkunguni kwa ustahamilivu wao
mkubwa kwa kipindi chote hicho cha miezi mitatu kufanya zoezi hilo bila ya
kujitokeza ukorofi wa aina yoyote juu urimbikaji huo.
Alieleza kwamba mashirikiano hayo ndiyo
yanayohitajika miongoni mwa jamii kwani ndio sababu kuu ya kuendeleza umoja na
mshikamano sambamba na kudumisha amani na usalama katika jamii.
Aliongeza kuwa pale panapojitokeza
wananchi wakorofi na kutofuata matakwa ya makubaliano juu ya zoezi hilo wakati
mwengine hupelekea kujitokea viashiria vya uvunjaji wa amani jambo ambalo
halipewi nafasi katika Wilaya hiyo.
Kutokana na mafanikio hayo, Mkasaba
aliwaeleza wananchi hao kwamba Ofisi ya Wilaya hiyo imeamua kwa makusudi kwamba
hivi sasa suala zima la urimbikaji wa pweza katika ukanda huo lisimamiwe na
Wilaya kwa lengo la kufuata taratibu na miongozo inayotolewa na vijiji husika kupitia
Kamati zao juu ya urimbikaji sambamba na uvunaji wa pweza.
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia
kuondoa migogoro inayotokea kati ya kijiji na kijiji katika zoezi zima la
kurimbika na kurimbua pweza.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya
Muyuni Mustafa Haji amesema kuwa mashirikiano mazuri kati ya wananchi na Kamati ya uvuvi ya kijiji
hicho ndio iliyopelekea kufanikisha zoezi hilo na kwa kiasi kikubwa imeonesha kufanikiwa kuwafunga pweza na
hatimae kuwavuna kwa wingi na wananchi kujiingizia kipato ili kuweza kujikimu
kimaisha.
Nao wananchi wa kijiji hicho cha
Kizimkazi Mkunguni kwa upande wao walitoa shukurani na pongezi kwa Mkuu huyo wa
Wilaya kwa mashirikiano mazuri anayowapa kwani amekuwa mstari wa mbele
kushirikiana nao katika jitihada zao za kujiletea maendeleo endelevu katika
kijiji chao.
Wananchi hao waliahidi kuendelea kumuunga
mkono Mkuu wa Wilaya huyo pamoja na uongozi wote wa Wilaya hiyo huku wakiwataka
wananchi wa kijiji hicho kuendeleza umoja na mshikamano walionao katika
shughuli zao mbali mbali za maendeleo zikiwemo hatua hizo za kuimarisha uchumi
wa buluu.
Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini,
Mkoa wa Kusini Unguja.
26.10.2022.
No comments:
Post a Comment