Habari za Punde

Zimamoto Yatoa Elimu na Ufafanuzi wa Dhana ya Kufika Kwenye Matukio Bila ya Maji

 

Sajini wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bahati Lugodisha, akitoa elimu kwa Wakazi wa Mjini Geita pamoja na maeneo jirani ambao wameendelea kutembelea Banda la Jeshi hilo kwa lengo la kupata elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga mbalimbali, katika Maonesho ya Tano ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Tanzania 2022, yanayoendelea katika Viwanja vya Bombambili Mjini Geita huku yakiwa yamebeba Kauli Mbiu “Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu”.

Sajini wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bahati Lugodisha, akitoa elimu ya namna Gari (mtambo) wa Zimamoto unavyofanyakazi unapofika kwenye tukio la moto, kwa Wananchi waliotembelea banda la Jeshi hilo mapema leo katika Maonesho ya Tano ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Tanzania 2022, yanayoendelea katika Viwanja vya Bombambili Mjini Geita huku yakiwa yamebeba Kauli Mbiu “Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu”.

Jeshi la Zimamoto la Zimamoto na Uokoaji ni moja kati ya wadau wanaoshiriki katika Maonesho ya Tano ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Tanzania 2022, yanayoendelea katika Viwanja vya Bombambili Mjini Geita huku yakiwa yamebeba Kauli Mbiu “Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu”.                                                                                       

Jeshi hilo limetumia nafasi hiyo kutoa ufafanunuzi na elimu kwa Wananchi waliotembelea Viwanjani hapo kuhusu dhana ya Jeshi hilo kufika kwenye matukio bila maji.

Akitoa elimu kwa Wananchi waliotembelea Maonesho hayo, Sajini wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bahati Lugodisha amewaeleza kuwa Jeshi hilo muda wote lipo tayari kutoa huduma ya kuzima moto na kufanya uokoaji, pia amesisitiza magari hayo huwa yamejazwa maji wakati wote yanapokuwa Vituoni yakisubiri matukio.

Aliongeza kuwa Gari la Zimamoto linapofika kwenye tukio hufanya kazi kama mtambo wa kuzimamoto, magari hayo yanamatanki ya maji yenye ujazo kuanzia lita 1,500 hadi lita 7,000 (kuna mengine hubeba lita 10,000). Utendaji kazi wa magari ya Zimamoto (mitambo), ili maji yatoke kwa nguvu na kuweza kuzimamoto, yamefungwa pampu zenye uwezo wakusukuma lita 1,000 hadi lita 6,000 kwa dakika itategemea umetumia mfumo upi.

Kwa kawaida tunapofika kwenye tukio hutumia mipira yenye kipenyo cha milimeta 70 na kufunga kifaa cha kumwagia maji (branch pipe) chenye kipenyo cha milimeta 20 na pampu husukuma maji kwa nguvu ya bar 7. Tukitumia vipimo hivyo huwa tunamwaga lita 1,000 kwa dakika kwa njia moja ya kutolea maji hivyo kwa gari lililobeba lita 7,000 maji yatakwisha ndani ya dakika saba.

“Endapo tukio la moto likiwa kubwa tunatumia njia mbili za kutolea maji hivyo huwa tunamwaga lita 2,000 kwa dakika, na gari lililobeba lita 7,000 maji yatakwisha baada ya dakika 3½ tunalazimika kuondoka eneo la tukio kwenda kutafuta maji”. Alisema Sajini Lugodisha

Sajini Lugodisha amewaelezea Wananchi hao, ili kuondokana na dhana hiyo, inatakiwa maji ya dharura au visima maalum vya Zimamoto (fire hydrants) yapatikane katika maeneo mbalimbali ambapo gari la Zimamoto likifika wakati wa dharura ya janga la moto liweze kuunganisha maji huku linaendelea kuzima moto.

Changamoto iliyopo ni ukosefu wa maji ya dharura kwenye mitaa na majengo ndiyo maana Wananchi wengi kuwa na dhana kuwa magari ya Zimamoto huenda kwenye matukio bila maji.   

Amewataka wananchi wajue kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeundwa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa jamii. Hivyo basi mtu yeyote anastahili kupata huduma hiyo kwa kupiga namba ya simu ya dharura 114 pindi kunapotokea dharura ya janga la moto au uokoaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.