Habari za Punde

Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii Zaagizwa Kutenga Nafasi za Mafunzo kwa Vitendo kwa Wanafunzi wa NCT

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) akikabidhi cheti cha pongezi kwa kufaulu vizuri kwenye masomo Mhitimu wa Diploma in Event Management, Salome Maiga wakati wa mahafali ya 20 ya Chuo Cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja (Mb), ameziagiza taasisi za Wizara yake kutenga nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kila mwaka ili kuendana na kasi ya ongezeko la wanafunzi na kuchangia upatikanaji wa maeneo ya mafunzo kwa vitendo sambamba na kutoa ajira kwa wanafunzi hao pale nafasi zinapopatikana.                                                                                                                      

Ameyasema hayo katika mahafali ya ya 20 ya Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa maendeleo ya utalii kitaifa yataweza kufikiwa endapo wadau wote watashiriki katika jitihada za kuelimisha, kuendeleza, kukuza na kuitangaza Tanzania na kwamba kwa kuboresha huduma bora za utalii kutaongeza tija katika sekta hiyo.

“Hatuna budi kuhakikisha kuwa huduma mbalimbali za utalii zinazotolewa zinabeba weledi unaostahili. Weledi huu utaonekana vizuri zaidi katika huduma zetu endapo tutaajiri wataalam wenye ujuzi stahiki kama wanaohitimu leo hii” Mhe. Masanja amesema.

Aidha, ametoa rai kwa wadau wa sekta ya utalii nchini kuhakikisha kuwa huduma mbalimbali za utalii zinazotolewa zinabeba weledi unaostahili na kwamba hilo litaonekana vizuri zaidi kwa vitendo endapo wataajiri wataalam wenye ujuzi stahiki kama wanaohitimu katika chuo hicho.

“Ifike mahali nchi yetu tujivunie kutoa wataalam wanaotosheleza soko la ndani na kupata fursa ya kutoa huduma katika soko la nje kama ilivyo kwa jirani zetu” amesema.

Sambamba na hilo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya jitihada za kuhakikisha utalii unaimarika ikiwemo uzinduzi wa Royal Tour ambayo imeleta hamasa kubwa kwa wageni na wenyeji.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey, amewataka wahitimu hao kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo ya utumishi wa umma wakatapokuwa wakitimiza majukumu yao wakiwa kazini.

Mahafali hayo yamehudhuriwa na Mabalozi, Wakuu wa Taasisi mbalimbali,Wadau wa Sekta ya Utalii na Ukarimu, Watumishi na Wanachuo,

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Mary Masanja (Mb) (wa pili kutoka kulia)akiwa katika maandamano ya mahafali ya 20 ya Chuo Cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam. Wengine ni menejimenti ya Chuo Cha NCT.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) (wa pili kulia) na Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii(NCT),Dkt.Florian Mtey (wa tatu kutoka kulia) na Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Bw.Imani Kajula  (kulia) na  Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Shughuli za Kitaalam, Bi.Jesca Willliam (kushoto) wakifurahia vikundi vya ngoma vilipokuwa vikitumbuiza katika mahafali ya 20 ya Chuo Cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Mary Masanja (Mb) akikabidhi cheti cha pongezi kwa kufaulu vizuri kwenye masomo Mhitimu wa Diploma in Hospitality Management, Furaha Pambe wakati wa mahafali ya 20 ya Chuo Cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) (kulia) akionyesha zawadi ya picha aliyokabidhiwa na mwanafunziwa wa Chuo cha Taifa cha Utalii katika kozi ya Basic Technician Certificate in Event Management Glory Siame wakati wa mahafali ya 20 ya Chuo  hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.