Picha na Miza Othman- Maelezo Zanzibar.
Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar, 14/12/2022.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban amesema utumiaji wa mifumo ya biashara utasaidia kukuza biashara na kurahisisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa ndani na nje ya Nchi .
Ameyasema hayo katika ukumbi wa ZURA, Maisara wakati akifungua mafunzo ya utumiaji wa Mifumo ya Biashara Zanzibar kwa viongozi wa umma na Taasisi Binafsi zinazohusiana na biashara.
Amesema hatua hiyo ni kubwa katika kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya Dunia kwa kufuata mfumo wa kibiashara ili kurahisisha kukuza biashara pamoja na kupata masoko kwa urahisi ya ndani na nje ya nchi .
Aidha alisema mfumo huo utasaidia kupata taarifa mbali mbali ikiwemo za masoko ya biashara za kimataifa kupata vibali, leseni na kujua vigezo vya biashara pamoja na kufanya maamuzi sahihi ya nchi ambazo zinatoa bidhaa bora.
Waziri huyo aliwataka viongozi hao kusimamia mfumo huo na kuwaeleza wafanyabiashara jinsi ya mwenendo wa soko duniani pamoja na kushuka na kupanda kwa bei za bidhaa.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Rashid Ali Salim amesema mfumo wa uwezeshaji biashara zinasimamiwa na mamlaka ya maendeleo ya biashara Tanzania TanTrade .
Alifahamisha kuwa TanTrade ni chombo cha serikali chenye mamlaka ya udhibiti utendaji na ushauri wa kuendeleza na kukuza biashara za ndani na nje ya nchi .
Alieleza kuwa dhima ya mamlaka hiyo ni kuwezesha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kuendeleza na kukuza bidhaa na huduma mbal mbali kwa masoko ya ndani na je ya nchi .
Kwa Upande wa Mkufunzi wa Mafunzo hayo Mshauri wa Mfumo wa Taarifa za Biashara TanTrade,Gema Mwikoko amesema iko haja ya Wakuu wa Taasisi kuwashajihisha wafanya biashara kujisajili katika mfumo huo ambao utawapatia mbinu za kibiashara pamoja na kupata masoko ya kikandana na kimataifa.
No comments:
Post a Comment