Habari za Punde

Vijana wa Kitanzania Kupata Fursa Marekani

 
Na Shamimu Nyaki

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul leo Januari 13, 2022 jijini Dar es Salam, ameongoza kikao kati ya Wizara hiyo na Wadau wa Diaspora kutoka nchini Marekani kupitia NGO ya Global Youth Support Center, kujadili nia ya NGO hiyo kupata vijana wa kitanzania wa umri kati ya Miaka 14 hadi 15 wenye vipaji mbalimbali vya Michezo na Sanaa kwa lengo la kwenda nchini Marekani kuendeleza vipaji vyao.

Katika kikao hicho, Naibu Waziri Mhe.Gekul amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora kwa wadau wa Sekta za Wizara hiyo kuwekeza kwa vijana wenye vipaji, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuongeza elimu itakayowasaidia katika kukuza uchumi wao na jamii.

"Hii ni fursa muhimu sana kwa vijana wetu, Wizara yetu ipo tayari kutoa ushirikiano wa karibu kwa Taasisi hii ili vijana wa Kitanzania waweze kunufaika na mpango huu wa kuendeleza vipaji” amesisitiza Mhe. Gekul.

Mratibu wa programu hiyo Bw. Oswald Bwechwa ameeleza kuwa, vijana takribani 40 watapata fursa ya kwenda nchini Marekani katika awamu ya kwanza ya programu hiyo.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa na la Taifa Dkt, Kedmon Mapana, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dkt. Kiagho Kilonzo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Neema Msitha na Waziri na Mbunge wa zamani nchini Kepten Mstaafu John Chiligati.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.