Habari za Punde

Wahitimu wa Vyuo Vikuu Nchini Kujikita Kwenye Tafiti Zitakazotoa Ufumbuzi wa Matatizo Yaliomo Kwenye Jamii

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait Zanzibar wakati wa mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya chuo Chukwani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 21-1-2023

NA MWASHAMBA JUMA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kujikita kwenye tafiti zitakazotoa ufumbuzi wa matatizo yaliomo kwenye jamii.

Aidha, alivitaka vyuo vikuu kuongeza progam kwa mujibu wa mahitaji ya wakati uliopo  na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani ili kuleta kuleta mabadiliko nchini

Dkt. Mwinyi alitoka kauli hizo kwenye Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al- Sumait, Chukwani Wilaya ya Magharibi B, Unguja.

Aliwataka wahitimu wa chuo hicho kutumia tafiti zao kwa lengo la kutatua changamoto zilizomo kwenye jamii badala kuziweka tafiti hizo kwenye makbtaba na kuzifungia.

Alizishauri Wizara na Idara za Serikali kushirikiana na vyuo vikuu kufanya tafiti zenye kuchochea maendeleo kwenye nyanja zote za jamii na uchumii, tehama na mawasiliano ili kutela  mabadiliko yenye tija.

“Nazishauri Wizara na Idara za Serikali kushirikiana na wataalamu wa vyuo vikuu vyetu, kufanya tafiti zitakazosaidia kuchochea maendeleo katika nyanja za kijamii, uchumi na teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuendelea kusonga mbele” Alishauri Rais Mwinyi.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi, aliwasihi wahitimu hao kwa watakao bahatika ajiriwa ama kujiajiri wenyewe baada ya kuhitimu mafunzo yao, wakafanyekazi kwa uadilifu, kujituma na kuchunga maadili mema yanayokubalika katika jamii ili waongeze tija kwa kuleta mabadiliko kwenye utendaji wao.

Aidha, aliwataka wakawe wabunifu wa kuzitafuta fursa za kujiendeleza zaidi na kuzitumia kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu kwa lengo la kujiimarisha kitaaluma.

Hata hivyo, aliwaasa wanafunzi wanaoendelea na masomo chuoni hapo kuendelea kudumisha nidhamu na kufuata mazuri ya watangulizi wao kwa kuwa na maadili mema ya kutafuta elimu ili wapate ufaulu mzuri

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa aliwataka wahadhiri wa chuo hicho kujikita zaidi kwenye kutoa elimu ya ufundi na mafunzo ya amali ili kuwapa uwezo wanafunzi wakujiajiri wanapokamilisha masomo yao.

Alisema Sera ya elimu inawataka wanafunzi watakapomaliza masomo yao yalazima kwa ngazi ya sekondari, kuwe na sehemu ya wao kupata kujiendeleza kwa ustadi na ufundi.

Alisema Serikali inania ya kutanua wigo kwenye skuli za umma kwaajili ya wanafunzi kujikimu pamoja na kuwana taasisi ama vyuo vitakavyo wawezesha wanafunzi kujiari baada ya mafunzo yao.

“Lazima tuwe na taasisi, tuwe na vyuo mbalimbali vyenye kutoa fani tofauti ambazo wanafunzi wataweza kujiajiri  baada ya masomo yao” Alishauri Waziri Lela.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele zaidi kwenye mafunzo ya Amali ili kuwapa uwezo wanafunzi wanaomaliza masomo yao wajirike.

Alisema kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Sumait kumekua msaada mkubwa katika kuendeleza juhudi za Serikali.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Msafiri Mshewa aliwataka wahitimu hao  wakasaidie kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao kwa kuutumia vizuri ujuzi wa taaluma zao kuongeza tija, aidha, aliwataka wakawe mabalozi na kuzikimbilia fursa kwa  kuzifanyia kazi zenye tija.

“Ni matumaini yetu elimu mliyoipata itawanufaisha nyinyi, jamii na Watanzania kwa ujumla, kila mmoja wenu anawajibu na nafasi ya kuchangia maendeleo  kwa kuangalia eneo la taaluma yake litakavyosaidia kuleta mageuzi ya maendeleo kwa kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe” Aliwaasa wahitimu hao.

Chuo cha Abdulrahman Al Sumait chini ya uongozi wa Mkuu wake, Dk. Aman Abeid Karume, Rais Msaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya sita, kina jumla ya wanafunzi 4553 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1998. Jumla ya wahitimu 310 wakiwemo wanawake 183 na wanaume 127 walikamilisha masomo yao na kuhuduria kwenye mahfali ya 22 ya chuo hicho

Wahitimu 18 kati yao walitunukiwa shahada ya udhamili, 241 shahada ya kwanza na 51 walitunukiwa stashahada na astashahada.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.