Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis
akipanda mti katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT)
kilichopo Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
“Soma na Mti” iliyofanyika chuoni hapo jana.
Mkuu
wa Wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza, Amina Makilagi akipanda mti katika
viwanja vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kilichopo Wilaya ya
Nyamagana mkoani Mwanza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Soma na Mti”
iliyofanyika chuoni jana.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis
akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza mara baada ya kushiriki zoezi
la upandaji miti wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya “Soma na Mti” iliyozinduliwa jana.
Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa
wizara na taasisi katika sekta za umma na binafsi kutumia nishati mbadala ili
kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa
Mhe. Khamis amesema hayo
Februari 25, 2023 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Soma na Mti’ katika Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Agustino jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha
upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika taasisi za elimu ya juu nchini.
Amesema zoezi la upandaji
katika maeneo mbalimbali nchini ni ajenda ya kitaifa inayoongozwa na viongozi
wa kitaifa akiwemo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe.Dkt
Philip Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na hivyo kuzitaka taasisi za
umma na binafsi kuunga mkono juhudi hizo.
“Tupo hapa kutekeleza
mpango wa Serikali juu ya utunzaji wa mazingira ikiwa ni muendelezo wa juhudi
zilizoanzishwa na viongozi wetu wakuu wa kitaifa. Nitoe rai kwa viongozi wa
ngazi zote kuhakikisha tunasimamia maelekezo ya Serikali ya kuzuia ukataji
miti, tuanze kutumia nishati mbadala kama gesi kwa ajili ya kupikia kama
anavyosisitiza Rais wetu,” amesema Mhe. Khamis
Aidha naibu waziri huyo
ametoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa
wanasimamia na kuendeleza kampeni hiyo kwa kuhakikisha kila shule na kila
mwanafunzi anakuwa na mti wake na kuhimiza utamaduni wa kila Kaya kupanda miti
na kila mtu anayenunua eneo kuhakikisha amepanda miti katika eneo lake.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi amesema suala mazingira ni moja ya
kipaumbele vya msingi kinachotekelezwa na taasisi zote za umma na binafsi
zilizopo katika Wilaya hiyo na kukusudia kulifanya Jiji la Mwanza kuendelea
kuwa Jiji la kijani.
“Katika Wilaya ya
Nyamagana kila mradi unaotekelezwa unafungamanishwa na mazingira na kila tukio
tunapanda miti na hivi karibuni taasisi zetu za TFS, Gereza la Butimba na wadau
wengine tulipanda zaidi ya miti 7000 katika vyanzo mbalimbali vya maji ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la Mhe. Makamu wa Rais,” amesisitiza Makilagi.
Ameongeza kuwa kupitia
kampeni ya “Soma na Mti” wilaya hiyo imejipanga kimkakati katika kuhakikisha
kuwa inafikia lengo la kupanda miti 1,500,000 kwa kushirikisha shule za msingi,
sekondari na taasisi za elimu ya juu na kuhakikisha inarejesha hadhi ya Jiji la
Mwanza kuwa kinara wa usafi wa mazingira nchini.
Naye Balozi wa Mazingira
Nestory Mushi amesema kupitia taasisi yake ya Mweka Site wamefanikiwa kuotesha
miti zaidi ya 358,000 na miti hiyo inatarajia kupandwa katika Mikoa yote
inayokabiliwa na hali ya ukame.
Taasisi yetu inahamisha
jamii katika shughuli zote za usafi wa mazingira ikiwemo upandaji miti na usafi
wa fukwe mbalimbali. Tunafundisha wanafunzi wa ngazi mbalimbali ikiwemo shule
za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuhusu vitalu vya miti, miradi ya samaki na
utunzaji mazingira” amesema Mushi.
Mwakilishi wa Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Alex Julius amesema katika kuunga mkono juhudi
za Serikali kuhamasisha utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji, TFS imeanzisha
kitalu cha miti ya matunda na vivuli ambapo kati ya Julai 2022 hadi Februari
2023, TFS imefanikiwa kuzalisha miche ya miti 67,310.
Wakati wa kuzalisha miche
hii tunazingatia masuala mbalimbali ikiwemo miche inayokuwa haraka, miche
inayohifandhi maji, miche inayozuia mmomonyoko wa udongo na kuanzia mwezi Julai
2022 hadi Februari 2023 miche ya miti 32,970 imegawiwa bure katika taasisi
mbalimbali” amesema Julius.
Kampeni ya “Soma na Mti”
ilizindiliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2022 ikiwa imelenga kuhamasisha
wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuona zoezi la upandaji
miti kuwa sehemu muhimu ya maisha ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko
ya tabianchi.
No comments:
Post a Comment