Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali pamoja
na Majaji walioshiriki Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Sheria Tanzania yaliyofanika
tarehe 1 Februari, 2023 katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali leo tarehe mosi Februari 2023 imeshiriki kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku ikiwakilishwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Duncan Mwaipopo pamoja na Mawakili wa Serikali.
Akizungumza
katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali
jijini Dodoma yenye kauli mbiu isemayo, “Umuhimu wa Utatuzi wa migogoro kwa
njia ya Usuluhishi katika kukuza uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau”,
Mhe. Rais Dkt. Samia amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Mahakama ya
Tanzania pamoja na wadau wake kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanatoa haki kwa
usawa na kwa wakati.
Mhe.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa yamechangiwa na
uamuzi wa Serikali iliyouchukua mwezi Agosti 2022 wa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu kutoka Majaji 78
waliokuwepo hapo awali mpaka kufikia Majaji wa Mahakama Kuu 100 hatua ambayo
imeongeza chachu katika kufikia mafanikio hayo leo.
Rais
Dkt. Samia ameeleza kuwa kwa sasa Majaji wote nchini wanaendelea kutoa haki kwa
usawa na wakati ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za
utoaji haki nchini pasipo kumuonea mtu yoyote.
Aidha,
Rais Dkt. Samia ameipongeza Mahakama kwa ujenzi wa miundombinu na kuendelea
kusogeza huduma karibu na wananchi huku akionyesha kufurahishwa zaidi na hatua
zilizofikiwa za kukamilika kwa taratibu za upatikanaji wa huduma za Mahakama
Kuu katika Mikoa minane ya Singida, Pwani, Songwe, Katavi, Geita, Njombe,
Simiyu na Lindi sambamba na mpango wa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki
katika maeneno mengine ikiwemo kisiwani Pemba.
Kuhusu
suala la upungufu wa watumishi pamoja na maslahi kwa watumishi wa Mahakama,
Mhe. Rais Dkt. Samia ameahidi kuendelea kulifanyia kazi suala hilo kwa kuanza
na hatua ya kuunda Kamati ambayo itakuwa na jukumu la kufanyia kazi suala hilo na
baadae itatoa taarifa yake baada ya miezi minne.
Mhe.
Rais Dkt. Samia ameeleza kutambua uwepo wa fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo
ikiwepo Benki ya Dunia ambazo zimesaidia kuimarisha miundombinu ya Mahakama,
ikiwemo Mahakama za Mwanzo 60 na majengo mengine 18 ambapo kati ya hayo ni
Mahakama 11 Wilaya.
“Uwepo
wa majengo haya ni ishara nyingine na azma ya Mahakama pamoja na Serikali
kuhakikisha inasogeza huduma za haki karibu na wananchi hivyo naomba kutoa rai
kwa uongozi wa Mahakama kuwa miradi yote inayotekelezwa izingatie ubora
unaoendana na fedha iliyotolewa,”, alisema Mhe. Rais Dkt. Samia
Mhe.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa azma ya Serikali yake kuhakikisha taasisi
zinazoshirikiana na Mahakama katika mnyororo wa utoaji haki, ikiwemo Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali zinapata pia miundombinu wezeshi ili shauri
linalofunguliwa Mahakamani linasomeka sawa sawa na lile lililosajiliwa katika
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Naye
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wananchi pamoja
na wadau wenye migogoro kutumia njia ya usuluhishi badala ya kukimbilia
Mahakamani kwa kuwa tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha
Sheria ya Usuluhishi ya Mwaka 2020 (Arbitration Act, 2020) ambayo pamoja na
mambo mengine imeweka mifumo madhubuti ya usimamizi na uratibu wa usuluhishi
ikiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Usuluhishi Tanzania (Tanzania Arbitration
Center)
Naye
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alimuahidi Mhe. Rais
Dkt. Samia kuwa Ofisi yake na ile ya Wakili Mkuu wa Serikali wataendelea kusimamia
vyema mashauri yote kwa niaba ya Serikali ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro
kwa njia ya usuluhishi pamoja na kusimamia kwa karibu maelekezo aliyoyatoa
kuhusu jambo hilo ili kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi.
Hotuba
hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia ilisomwa na Mawakili wa Serikali
kwenye kilele cha maadhimisho hayo kwenye Mikoa yote ambayo ina Ofisi za
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali
Maadhimisho
hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama akiwemo Jaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye ndiye aliyekuwa
mwenyeji wa Maadhmisho hayo, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama,
Mhe. Wilbert Chuma pamoja na watumishi wengine.
Wageni
wengine walikuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Spika wa Bunge la Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt.
Damas Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu
wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha
Mawakili Tanganyika, Prof. Edward Hosea na wananchi kwa ujumla.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na viongozi na watumishi pamoja na
wananchi (hawapo pichani) walioshiriki sherehe za kilele cha Siku ya Sheria
nchini leo tarehe 01 Februari, 2023 katika Viwanja vya Chinangali jijini
Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisoma hotuba yake katika Sherehe za
Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Majaji wa Mahakama ya Rufani
na Mahakama Kuu ya Tanzania wakisikiliza hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan leo tarehe 01 Februari, 2023 katika
kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika
Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali
Mhe. Sarah Duncan Mwaipopo (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja
na Mawakili wa Serikali wa Ofisi yake kwenye maadhimisho ya Kilele ya Wiki ya
Sheria yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali Mhe. Sarah Duncan Mwaipopo akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu wa Wizara
ya Katiba na Sheria, Mary Makondo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya
Sheria yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Sarah Duncan Mwaipopo akiwa kwenye maandamano kwa ajili ya ufunguzi wa maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Sheria yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment