Habari za Punde

Pententiole Ndege Aliyehamia Kutoka Madagascar Kivutio Hifadhi ya Mwambesi Tunduru

Ndege jamii ya Pentiole ambaye utafiti umebani amehamia katika nkatika hifadhi ya Taifa ya Mazingira asilia Mwambesi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kutoka nchini Madagasca

MSITU wa Hifadhi wa Taifa wa mazingira asilia Mwambesi uliopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ulianzishwa mwaka 1956 na ulipandishwa hadhi kuwa msitu wa Taifa katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Meneja wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Tunduru Denis Mwangama anasema msitu huo umepandishwa hadhi ili kuongeza uhifadhi zaidi kutokana na kuwa na utajiri wa viumbe vya kipekee duniani wakiwemo wanyama,ndege na mimea.

Anawataja wanyama waliopo katika msitu huo ambao upo kando kando mwa Mto Ruvuma kuwa ni simba, tembo, chuo,kuro,jamii za nyani,jamii za swala,nyati na wanyama wengine.

Mwangama anasema Katika msitu wa Mwambesi kuna jamii ya ndege maarufu duniani anayeitwa Pentiole ambaye utafiti uliofanywa na PALMS Foundation mwaka 2015 umebaini kuwa ndege huyo amehamia kutoka nchi ya Madagaska baada ya mazingira aliyokuwa anaishi kuharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Kwa mujibu wa Mwangama, ndege huyo ana tabia ya kuzamia samaki kutoka majini na kwamba ndege hao wanapenda kuishi kwenye maporomoko ya  Mto Ruvuma yanayoitwa sunda ambayo yapo ndani ya hifadhi hiyo.

“Tanzania tuna bahati katika msitu wetu tuna ndege Pentiole ambaye  amekuwa akiishi ukingoni mwa maporomoko ya maji yajulikanayo kama Sunda Water falls’’,anasisitiza.

Kwa mujibu wa Mwangama Ndege huyu huogolea kwankufuata mdondoko wa  mawimbi ya maji  kwenye maporomoko hayo akitatafuta mawindo yake ya samaki ambacho ndicho chakula chake pekee.

Licha ya ndege huyo Mwangama anayataja maporomoko ya Sunda kuwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii katika hifadhi ya Mwambesi na kwamba maporomoko hayo yalitumika wakati wa vita ya  Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907 ili  kujificha kwenye mapango kwa juu.

Anasema Mto huo ndio uliokuwa ukitumika kwenye vita vya Majimaji ambapo watu wa makabila au ukanda  wa kusini hususani  Wangoni walitumia maji yake katika kuzimia silaha za moto chini ya uongozi wa Kinjeketile Ngwale.

Kulingana na Mwangama, eneo hilo pia linaaminika Wajerumani walitumia kama njia kubwa wakitokea Msumbiji katika biashara ya meno ya Tembo na kwamba Waarabu walipita pembezoni  mwa mto huo  kuwapitishia watumwa.

Hata hivyo anasema awali kabla ya serikali kuamua msitu huo kuwa Msitu wa hifadhi,kulikuwa na vitalu vya uwindaji wa kitalii ambapo ndani ya msitu kulikuwa na kambi ya wawindaji iliyoitwa Big Game iliyoendeshwa na   Kampuni ya  uwindaji iliyoitwa Tandara Hunting Safaris.

Kulingana na Meneja huyo,msitu huo una ukubwa wa zaidi ya hekta 112,000 na kwamba mtalii akiwa katika msitu wa Mwambesi anaweza kufanya utalii wa kuteleza kwenye mitumbwi katika mto Ruvuma.

Deborah Mwakanosya ni Meneja wa Msitu  anasema Mwambesi ni msitu wa asili wa pili kwa ukubwa kwa Tanzania ukiongozwa na msitu wa Kilombero mkoani Morogoro.

Anasema msitu huo ambao umezungukwa na mto Ruvuma, umesheheni baianowai mbalimbali za mimea adimu duniani ikiwemo miti aina ya mipozipozi ambayo ina tabia ya kudondosha maji inapatikana sehemu chache duniani ukiwemo msitu wa Mwambesi.

Mwambesi ni moja kati ya Misitu mikubwa ya Hifadhi za Mazingira Asilia tulionayo wenye utajiri mwingi wa flora na fauna zakutosha.

Msitu wa Mwambesi unahifadhiwa kisheria chini ya uangalizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania  kwa kushirikina na  Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Kusini.

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. 

Baadhi ya watalii wa nje ya nchi wakiwasili katika hifadhi ya Taifa ya mazingira asilia Mwambesi wilayani Tunduru
Meneja wa Huduma za Misitu Tanzania TFS Wilaya ya Tunduru Denis Mwangama
Ufukwe za Mto Ruvuma ndani ya hifadhi ya Mwambesi moja ya maeneo ya kuvutia watalii wanaotembelea hifadhi hiyo inayopakana na nchi ya Msumbiji
Mapomoroko ya Sunda katika Mto Ruvuma  ndani ya hifadhi ya Mwambsi ambako ndege huyo anapenda kuishi kwa kula samaki ambacho ndicho chakula chake kikuuu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.