Habari za Punde

Taasisi za Dini Zina Mchango Mkubwa kwa Serikali

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Hindi Sunni Jamaat Zanzibar, ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Nizar Mohammed (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kumpongeza leo 2-2-2023, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Taasisi za dini zina mchango mkubwa kwa Serikali hasa kwenye jukumu zima la kuendeleza amani Zanzibar.

Alisema taasisi hizo ndizo zinazowalea vijana kiimani, weledi, ujasiri na uzalendo kwa taifa na viongozi wao jambo ambalo linaimarisha amani na uthubutu wa kufikia maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na uongozi wa  Jumuiya ya Sunni Jamaat waliofika kujitambulisha.

Alisema taasisi binafsi na za kidini zinajukumu la kuisaidia Serikali kuendeleza huduma za jamii pia aliishukuru jumuiya hiyo kwa juhudi za kuendeleza elimu Zanzibar.

 Aidha, alizitaka jumuiya za dini kuendelea kuishauri Serikali kwa mawazo yatakayojenga na kuleta ufanisi kwenye misingi ya maendeleo ya taifa, hata hivyo aliishukuru taasisi hiyo kwa mchango wanaoutoa kwenye sekta ya elimu.

Dk. Mwinyi alizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya elimu zikiwemo uhaba wa vifaa vya maabara, maktaba, kuongeza madawati, kompyuta na vitabu, pia kuondoa mikondo kwa wanafunzi. Hata hivyo, alisema Serikali ya awamu ya nane imejenga skuli 48 kati ya hizo 10 za ghorofa.

“Kwa hatua tuliyofikia matokeo yanaweza yasionekane leo, maana ukianza kuigeuza elimu faida yake itaonekana miaka mingi baadae.” Alifaafnua Rais Mwinyi.

Alisema Serikali pia inafanya utafiti wa kina kutafuta suluhu ya wanafunzi wengi kufeli na kuweka mikakati imara itakayoinua sekta ya elimu, Zanzibar.

“Safari hii tumeamua kufanya utafiti maana changamoto za elimu ni nyingi mno kila kona huwezi kuziepuka, kuanzia idadi ya wanafunzi kwenye madarasa ndio maana tunajenga skuli mpya ili kupunguza idadi ya wanafunzi wengi madarasani” alifahamisha Dk. Mwinyi.

Alisema serikali pia inaangalia upya mfumo wa elimu ambao wanafunzi wengi huanza msingi lakini wanaoingia vyuoni ni wachanche hivyo inaangalia kundi la katikati linalofeli ambalo ni kubwa.

Wana Jumuiya hao walimshukuru Dk. Mwinyi kwa juhudi ya kuipambania sekta ya elimu nchini na kueleza kuwa wameshuhudia mafanikio makubwa ndani ya miaka miwili  ya uongozi wake hasa kwenye kutoa kipaumbele kuimarisha huduma za jamii .

Walitumia fursa hiyo kuusifu kwa uongozi wake mahiri ambao waliueleza kwamba unaendelea kudumisha amani niliopo.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.