Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar imesaini mkataba na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii wa kusaidia Usajili wa watoto kupata vyeti vya kuzaliwa.
Akizungumza leo Machi 31 wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo katika ofisi za Wizara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeda Rashid Abdullah amesema wataunda timu ya pamoja na Wakala huo kuhakikisha tatizo hilo linapata ufumbuzi.
"Kuna shida ya kuchelewa kuwasajili watoto wengi na kukosa haki zao za kupata vyeti vya kuzaliwa, kwahiyo tumeona kuna haja kuandaa mpango wa pamoja kuhakikisha tunashghulikia tatizo hili," amesema Katibu Mkuu
Amesema kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kuwa na uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa vyeti hivyo jambo linalowafanya wengine kupuuza lakini hupata changamoto wanapokuwa na mahitaji mengine yanalazimisha mhusika awe na cheti cha kuzaliwa.
Amesema wao ikiwa ndio wizara yenye dhamana na watoto wanawajibu kuhakikisha wanatoa elimu kwenye jamii kwa kushirikiana na ngazi zingine wakiwemo masheha.
Hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuona umuhimu na kuhakikisha watoto wao wanapatiwa vyeti halisi vya kuzaliwa.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii, Makame Mussa Mwadini amesema makubaliano hayo ya miaka mitatu yataleta matokeo chanya na kuhakikisha watoto wote ambao hawana vyeti hivyo na wanasifa za kuwa navyo wanavipata.
"Tunataka ifikapo mwaka 2030 pasiwepo na mtu ambaye hana cheti cha kuzaliwa wakati ana sifa zote," amesema
Mkurugenzi Ustawi wa Jamii na Wazee , Hassan Ibrahim Suleiman amesema wananchi wengi wamekuwa wakilalamika watoto kukosa vyeti vya kuzaliwa lakini kupitia makubaliano hayo wanaiman watapunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment