Habari za Punde

Puma Energy kushirikiana na Chuo cha Teknolojia cha Karume kukuza ujuzi wa sayansi na teknolojia Zanzibar

 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Zanzibar, Lela Mohammed (Kulia) na Afisa Mwendeshaji  Mkuu wa Puma Energy  Afrika , Ben Hassan Ouattara (Kushoto) wakishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah na Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST). ), Dk Mahmoud Abdulwahab Alawi. Kampuni ya Puma Energy Tanzania itawekeza shilingi milioni 352 kusaidia programu ya mafunzo ya wahitimu wa miaka mitatu yenye lengo la kuendeleza sayansi na teknolojia Zanzibar. Hafla hiyo ilifanyika Zanzibar.25-5-2023.

 Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, akipeana mkono na na Dk Mahmoud Abdulwahab Alawi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano ambapo Puma Energy Tanzania itawekeza shilingi milioni 352 kwa miaka mitatu kusaidia programu ya mafunzo ya wahitimu wa taasisi hiyo na Pamoja Zanzibar yenye lengo la kuendeleza sayansi na teknolojia Zanzibar.Hafla hiyo iliyofanyika Zanzibar.

 Wahitimu kutoka taasisi ya Karume Institute of Science and Technology (KIST) na Pamoja Zanzibar, watakaoshiriki katika programu ya Puma Energy ya kukuza sayansi na teknolojia Zanzibar katika picha ya pamoja na Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi wa zanzibar ,Mh. Lela Mohammed (katikati waliokaa) wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano iliyofanyika Zanzibar jana. Wengine pichani ni Meneja Mkuu wa Puma Energy nchini, Fatma Abdallah, (kushoto),Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Puma Afrika, - Ben Hassan Ouattara ( wa pili  kutoka kushoto),Mkurugenzi wa KIST, Dr. Mahmoud Abdulwahab Alawi (wa pili kutoka kulia) na Mkurugenzi wa Fedha wa Pamoja Zanzibar, Benjamin Kogel ( kulia).

Kampuni ya Puma Energy Tanzania,  imezindua ushirikiano wa mafunzo ya wahitimu wa  Taasisi ya Teknolojia ya Karume (KIST) na Pamoja Zanzibar. Programu hizo zinalenga kukuza ujuzi wa sayansi na teknolojia Zanzibar. Kama sehemu ya makubaliano hayo, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, kampuni ya Puma Energy Tanzania, itawekeza hadi dola 150,000 (TSh352 milioni) kuendeleza ujuzi na itatoa programu za mafunzo ya vitendo ili kuwasaidia wahitimu kupata ujuzi muhimu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Zanzibar, Bi Lela Mohammed ameupongeza mpango huu na kusema kuwa unaendana sambamba na  mkakati mpana wa Serikali ya Zanzibar katika kuendeleza uchumi wa Taifa.

“Ushirikiano kati ya Puma Energy, KIST, na Pamoja Zanzibar unathibitisha umuhimu wa ushirikiano wa umma na binafsi katika kuleta maendeleo endelevu. Serikali ya Zanzibar inathamini na kuunga mkono juhudi za sekta binafsi katika kuwekeza na kushirikiana na Serikali katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.”

 Programu ya wahitimu wa KIST itakayotolewa na Puma Energy Tanzania itaanza na wahitimu watatu wa KIST. Mpango wa Pamoja Zanzibar utalenga kukuza ujuzi wa huduma na matengenezo ya magari kwa wahitimu wengine wawili. Programu zote mbili zitafanyika katika kituo cha Puma Energy kilichopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni ya uwajibikaji kwa jamii Zanzibar, ambayo itawapa wahitimu fursa ya kuwa sehemu ya wafanyakazi wa kampuni. "Kama sehemu ya ratiba ya mafunzo, washiriki wa KIST watajifunza kuhusu uendeshaji na utendaji wa bohari zetu wa kila siku, na shughuli za matengenezo katika uwanja wa ndege na wahitimu wa Pamoja Zanzibar watajifunza kuhusu matengenezo ya magari."

Kwa kuanzia, wahitimu watano watakaoingia kwenye mafunzo watachaguliwa kwa mwongozo kutoka KIST na Pamoja na katika siku zijazo programu inaweza kupanuliwa ili kuchukua wahitimu wengi zaidi katika maeneo mengineyo ili kuweza kupata ujuzi katika kuendesha bohari  ya mafuta iliyopo  Mtoni  Zanzibar.

 Mwanzoni programu itaendeshwa katika kipindi cha mitatu na ikiisha kutakuwepo na uwezekano wa kuongeza muda.

“Puma Energy tayari imewekeza ili kuhakikisha mitambo yake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ni miongoni mwa viwanja vya kisasa, vyenye ufanisi na vya uhakika barani Afrika na sasa tunafanya uwekezaji huu mkubwa ili kukuza ujuzi na fursa kwa vijana wa Zanzibar. Kwa kufanya hivyo tunadhihirisha dhamira yetu kwa Tanzania, kuchangia ustawi wa Zanzibar na kuwapatia mustakabali mzuri wahitimu watakaojiunga na programu hiyo,” alisema Bi Abdallah.

“Programu ya wahitimu ya kampuni ya Puma Energy inatoa fursa nzuri kwa wahitimu wetu kutumia ujuzi walioupata katika Taasisi ya Teknolojia ya Karume katika mazingira ya kazi. Mpango huu wa mwaka mzima umeanzishwa kwa umakini ili kuwafundisha wahitimu watano ujuzi  watakaohitaji ili kuhimili  mazingira ya kazi na unatoa mwanya wa kuajiriwa kwa muda mrefu na kampuni kubwa ambayo ni kiini cha uchumi wa Zanzibar,” alisema Dk Mahmoud. Abdulwahab Alawi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume.

Mmoja wa wahitimu anayeshiriki katika programu ya mafunzo haya, Gulam Abdallah, alisema, "Nimefurahi sana kuchaguliwa katika programu ya wahitimu ya Puma Energy, ni fursa nzuri. Nimejifunza mengi katika Taasisi ya Teknolojia ya Karume na sasa natarajia kuweka ujuzi wangu kutumia na kujifunza zaidi kuhusu biashara ya usafiri wa anga kwa mwajiri mwenye viwango vya hali ya juu.”Mpango huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2030 ya kuwa na jamii iliyoelimika vizuri na kujifunza, na unampa mtu binafsi uwezo wa kuleta mabadiliko katika jamii zao kwa kushirikiana ili kufikia lengo la kuwa na jamii imara jumuiya na kujenga mustakbali mzuri kwa kizazi kijacho cha Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.