Na; Mwandishi Wetu - Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, ameongoza kikao cha wadau, kilichojadili kuhusiana na uendelevu wa Safari Channel.
Kikao hicho kilichofanyika tarehe 8 Mei, 2023 Jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine kimejadili namna ambavyo channel hiyo inaweza kupeleka matangazo yanayofaa kwa jamii, kuelimisha, kuburudisha na kuipeleka nchi nje ya mipaka ya Tanzania.
Aliongezea kuwa, hili litawezekana endapo wadau watashikana mkono, na kuhakikisha kwamba Tanzania inaonekana katika televisehni za mataifa mengine kwa kuzingatia ubora ambao unatangaza Nchi na kuendeleza uchumi.
Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Kakele aliwataka wadau kuendelea kushirikiana ili channel hiyo iendelee kuruka na kuitangaza Tanzania kiutalii kwa ujumla katika anga za kimataifa na kuchangia mapato ya serikali.
Akizungumzia nafasi ya Safari Channel katika muktadha wa kidiplomasia, Bw. Kakele alisema ipo dhana ya nguvu laini ya ushawishi wa nchi katika eneo la ukanda na Jumuiya za kimataifa.
“Sisi tunaamini Safari Channel ikifanya vizuri itatusaidia kama Tanzania kujitangaza na kueneza utamaduni na lugha yetu ya kiswahili, katika eneo la ukanda na kimataifa, na hilo litafanikiwa kwa kupitia maudhui yanayorushwa kupitia vipindi hivyo, na si tuu ya utalii bali pia katika eneo la utamaduni kwa ujumla wake lina mchango mkubwa sana katika kuitangaza nchi yetu.”Alisisitiza
Aliendelea kusema kuwa, ushawishi na kukubalika kwa muziki wa Tanzania katika eneo la Maziwa Makuu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Lugha ya Kiswahili na umaafuru wa wasanii waliopo ndani ya Nchi wanaonekana katika baadhi ya channel zinazoonekana katika ukanda huo.
“Tukiwa na Mkakati wa Kitaifa wa kushirikiana pamoja na wadau mbalimbali kupitia Safari Channel, tutaweza kuongeza ushawishi wetu katika eneo hili la Ukanda wa Maziwa Makuu, pengine na nje ya mipaka ya Maziwa Makuu.” Alibainisha Bw. Kakele
Kikao hicho kilihusisha baadhi ya Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi ambacho kililenga kujadili na kufanya tathmini ya uendeshaji wa Safari Channel.
No comments:
Post a Comment