Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande akijibu swali bungeni jijini Dodoma.
Na Farida Ramadhani, WFM – Dodoma.
Serikali imesema kuwa itaendelea kutoa ushirikiano kwa benki za biashara nchini kuanzisha kampuni tanzu nje ya nchi ili kusambaza huduma za kibenki katika nchi mbalimbali na kurahisisha ufanyaji wa biashara kati ya nchi na nchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kusini, Mhe. Nashon William Bidyanguze, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itashawishi mabenki kufungua Benki nchini Congo DRC katika Miji ya Kalemie na Uvira ili kurahisisha biashara.
“Mei, 2021 Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania iliipa benki ya CRDB kibali cha kufungua kampuni tanzu Lubumbashi, nchini Congo ambapo inatarajia kuanza kutoa huduma za kibenki mara tu itakapopewa leseni na Benki Kuu ya Congo”, alisema Mhe. Chande.
Alibainisha kuwa katika Mkakati wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa Mwaka 2023 - 2028 unaonesha kuwa benki hiyo inatarajia kufungua kampuni tanzu zitakazotoa huduma za kibenki kwenye miji ya Bukavu, Uvira na Kalemie nchini Congo.
No comments:
Post a Comment