Habari za Punde

Uongozi wa Benki ya NMB Wapongezwa kwa kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA)

Na.Mwandishi wa OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Uongozi wa Benki ya NMB kwa kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) katika kukuza uwekezaji na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mhe. Hemed ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

 

Amesema Serikali imeridhika na hatua ya NMB kuendelea kuwasaidia wananchi kupitia makundi mbali mbali ikiwemo kina mama wanaolima mwani sekta ambayo inawagusa wananchi wengi wenye kipato cha chini.

 

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeamua kujenga Kiwanda cha Kuchakata na kusarifu mwani ambapo juhudi za Benki hiyo kusaidia kina mama hao kwa kiasi kikubwa na kuwapa ari ya kuzidisha ulimaji wa zao hilo.

 

Aidha ameeleza kuwa hatua ya Benki hiyo kushirikiana na Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo zanzibar kutasaidia kukuza sekta hiyo nchini.

 

Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi huo kwa uamuzi wake wa kufungua matawi katika Mkoa ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na kuongezeka kwa Mawakala katika maeneo mbali mbali hatua ambayo itasaidia kutanua Wigo wa kibiashara wa huduma za kibenki Nchini.

 

Aidha ameupongeza Uongozi huo kwa kufanya maamuzi ya Kushirikiana na Serikali katika kuisaidia jamii kwenye masuala mbali mbali ya Kijamii na Kiuchumi.

 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna amemueleza Mhe. Hemed kuwa Benki hiyo inaendelea kufanya kazi zake Tokea kuasisiwa kwake Mwaka 1997 ambapo mtaji wake unaendelea kukuwa kwa kasi.

 

Aidha amezishukuru Taasisi mbali mbali za Serikali kwa kuendelea kuwaunga Mkono katika shughuli zao za kila siku na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa Benki hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.