Habari za Punde

Wanawake waaswa kuacha kutegemea viti Maalum - Wito

Mhadhiri chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) Dkt.Salim Suleiman Ali akizungumza na wanawake wanaotarajia kushika nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali vya siasa wakati akiwasilisha mada ya muongozo wa Sera ya Jinsia  kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar  (TAMWA) kupitia mradi wa kuwainua Wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL) huko Ofisi za Tamwa Tunguu Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini unguja,julai 20,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Baadhi ya Wanawake wanaotarajia kushika nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali vya siasa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo  yaliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar  (TAMWA) kupitia mradi wa kuwainua Wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL) huko Ofisi za Tamwa Tunguu Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini unguja,julai 20,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR MAELEZO YA PICHA

Mjumbe kutoka chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Chimbuni Mashavu Bakari Juma akichangia mada katika Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kugombea nafasi za Uongozi Wanawake wa Vyama mbalimbali vya Siasa yaliyofanyika kupitia mradi wa kuwainua Wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL) unaotekelezwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA),Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na PEGAO huko Ofisi za TAMWA Tunguu Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini unguja,julai 20,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Mwenyekiti wa Wanawake Taifa Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Safia Mussa Bebwa Juma akichangia mada katika Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kugombea nafasi za Uongozi Wanawake wa Vyama mbalimbali vya Siasa kugombea nafasi za Uongozi Wanawake wa Vyama mbalimbali vya Siasa yaliyofanyika kupitia mradi wa kuwainua Wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL) unaotekelezwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA),Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na PEGAO huko Ofisi za TAMWA Tunguu Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini unguja,julai 20,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR

Wanawake katika jamii wametakiwa kuacha kutegemea Viti maalum na badala yake kuwa tayari kuingia katika ushindani wa kushika nafasi za uongozi sawa na Wanaume.

Akiwasilisha mada ya muongozo wa Sera ya Jinsia wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake wanaotarajia kushika nafasi za uongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa  Mhadhiri Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) Salim Sleiman Ali amesema ili  wanawake waweze kushika nafasi hizo ni lazima  kujipanga na kuweka mikakati madhubuti kabla ya kuingia katika ushindani.

Akielezea baadhi ya mbinu za kuwajengea ujasiri wa kupambania nafasi hizo amasema ni pamoja na kujua fursa za maendeleo ili kuweza kuzitumia katika kuishawishi  jamii  kuweza kuwakubali.

Vile vile aliwataka kujiunga na makundi ya kisiasa kabla ya kuingia majimboni na katika wadi ili kujenga  mazowea kati yao na Viongozi wazoefu pamoja na wajumbe wanaotarajia kuwachagua kushika nafasi hizo.

Aidha alieleza kuwa kutambua changamoto za eneo husika analotaka kuongoza kutamwezesha mwanamke huyo  kujua wapi aanzie kuweza kuishawishi jamii kukubali  kumchagua .

Amesema ili uwe kiongozi Bora ni lazima ukumbane na changamoto mbalimbali  hivyo aliwataka kuzitumia changamoto hizo kuzigeuza kuwa fursa.

Vile vile aliwashauri Wanawake hao kuwa na mazowea na wanahabari ili kuweza kujitangaza sambamba na kujizowesha kutumia mitandao ya kijamii kwa kutafuta fursa mbalimbali kwaajili ya maendeleo yao na watakaowaongoza.

Hata hivyo aliwataka kujiweka katika muonekano mzuri ili kuwa kivutio kwa jamii yake kwani kuvaa na kujipamba kupitiliza kunapunguza hadhi ya kuwa kiongozi.

"Kiongozi anatakiwa awe nadhifu asiwe ni mwenye kuvaa mavazi ya gaharama na kujipamba kupitiliza , watu watakuwa hawana imani na wewe wakidhani uongozi wako ni kwaajili ya maslahi binafsi na si kwa maslahi ya jamii"

Nao Washiriki wa Mafunzo hayo wamesema kupitia  mafunzo hayo  wanatarajia kuleta mabadiliko makubwa ya jinsia hivyo  kuwataka wanawake wenzao kuacha kutegemea nafasi maalum za upendeleo na badala yake kujipanga kisera na kuweza kuingia katika ushindani wa kuchaguliwa.

Vile vile waliwashauri  wanawake wenzao kutokutumia fedha kama kishawishi cha kuweza kupata uongozi na  badala yake kujiamini na kutumia sera zinazotekelezeka na kuvutia kwa jamii iliyozunguka.

Waliongeza kwa kusema  imezoeleka kuwa adui wa kwanza wa Mwanamke  ni Mwanamke mwenzie hivyo walitumia fursa hiyo kuwataka wanawake hao kubadilika na kuwaunga mkono Wanawake wenzao hata kama watakua na mtazamo tofauti wa kisiasa.

Mafunzo hayo ya siku 3 yaliwashirikisha wanawake wanaotarajia kugombea nafasi za Uongozi kupitia vyama mbalimbali vya siasa chini ya  mradi wa kuwainua Wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL)  unaotekelezwa na  Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar  (TAMWA),Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na PEGAO.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.