Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Mwinyi Akabidhi Vyeti vya Shukrani Kwa Wadhamini ya Mwaka Mpya wa Kiislamu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Viongozi wa Dini na Wajumbe wa Kamati ya Mwaka Mpya wa KiislamuZanzibar , wakati wa kukabidhi Vyeti vya Shukrani kwa Wajumbe kamati hiyo, iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 21-8-2023

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasihi wadhamini na wadau wote walioungamkono maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam kutochoka kuendeleza juhudi zao kila mwaka wa maadhimisho hayo. 

Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam 1445 H yaliyoadhimishwa mwaka huu, kisiwani, Pemba kwa nia ya kuwashukuru.

Aliishukuru Kamati, viongozi wote wa dini pamoja na wadhamini waliochangia na kushiriki bega kwa bega hadi kufanikisha maadhisho hayo ya mwaka mpya wa kiislam 1445 H.

“Nichukue fursa hii kuwashukuru wadhamini wote wengine mpo hapa na hata waliokuwa hawapo, mkisikia tu tuna kushukuruni mjue tunakuhitajini tena, kwa hiyo msochoke sababu maadhimisho haya yatakua kila mwaka katika kuadhimisha mambo ya heri” alisihi, Al hajj Dk. Mwinyi.

Al hajj Dk. Mwinyi alieleza Serikali ilipokea kwa uzito mkubwa ombi la Kamati hiyo la siku ya mapumziko ya kitaifa kila ifikapo maadhimisho ya mwaka huo na kueleza shukarani zake kwa kamati hiyo kwa kuja na hoja hiyo ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa na kueleza tukio la ugawaji vyeti vya shukrani kwa kamati hiyo ni ishara ya kukubalika kwa hatua ya mafanikio waliyoikamilisha.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwl. Haroun Ali Suleiman, alishukuru ushirikiano uliopo baina ya Serikali na kamati hiyo hadi kufanikishwa kwa maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam 1445 H ambao alieleza kupokelewa vizuri kwenye jamii.

Naye, Mfti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi alimshukuru Al hajj Dk. Mwinyi kwa mwitikio wake na ushirikiano anautoa kwa Ofisi ya Mufti na kushiriki vyema kwenye mambo yenye heri.

Alisema, kuanzishwa kwa jambo hilo kitaifa ni neema kubwa ya kuendeleza mambo mema kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Akiwasilisha taarifa ya shukurani kwa Serikali kutokana na maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam 1445 H, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti, Sheikh Khalid Mfaume, alisema lengo la maadhimisho yam waka huo ni kuitangaza tarehe ya kiislam na kuendeleza historia ya dini walioiacha maulamaa na kuahidi ofisi ya Mufti inajukimu ya kuendelea kuitangaza tarehe hiyo kwa kuishajisha kwa jamii kuendelea kutenda mema.

Aliishuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuthamini maoni ya wananchi wake baada ya kupokea ombi ya siku ya mapumziko kila ifikapo siku maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislam kila mwaka.

Maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam 1445 Hijria, yaliadhimishwa masjid Munawwara, uliopo eneo la Mfikiwa Mkoa wa Kusini, Pemba ambako Mgeni rasmi alikua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al Hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi na kuhudhuriwa na viongizi wengine wa dini na kitaifa kwa kutanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo kutoa huduma za matibabu ya macho kwenye hospitali ya kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kusomwa dua ya kuliombea Taifa, kufanikishwa kwa kongamano kuwa la wanawake wa Kiislam lililohudhuriwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Hajjat Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye ukimbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege, Zanzibar, maonesho ya kiislam ya biashara yaliyowashirikisha wafanyabiasha wadogo na wajasiriamali, matembezi ya Zafa, kisiwani Pemba  yaliolenga kuboresha afya pamoja na matembezi ya hiari yalifanyika Unguja.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.