Habari za Punde

Kamati za Usimamizi wa Maafa Zatakiwa Kuchukua Tahadhari Mvua za El Nino

Naibu  Katibu  Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatebwa akizungumza wakati akifungua  Kikao Kazi cha Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na madhara ya El Nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa  kilichofanyika Mkoani  Pwani.
Baadhi ya washiriki wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa wakifuatilia Kikao Kazi cha  Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na madhara ya El Nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa  kilichofanyika Mkoani  Pwani.
Baadhi ya washiriki wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa wakifuatilia Kikao Kazi cha  Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na madhara ya El Nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa  kilichofanyika Mkoani  Pwani.

Na Mwandishi wetu- Pwani

Kamati za Usimamizi wa Maafa nchini  zimetakiwa  kuchukua hatua madhubuti  za  kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu  Katibu  Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatebwa wakati akifungua  Kikao Kazi cha Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na madhara ya El Nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa Mkoa wa Pwani ambapo amesema  matukio ya maafa yanatokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii ambapo Serikali za Mitaa, kuanzia Kitongoji, Mtaa au Kijiji na Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya zinawajibika kuhakikisha  usalama wa watu  kulinda mali za wananchi.

Amesema kila mmoja anawajibika kuchukua hatua katika eneo lake, akisema  mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi yenye jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali za jamii  kutokana na matukio ya maafa.

“Kikao kazi cha leo kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea,”Amesema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Hata hivyo amezitaka taasisi zinazohusika   kujiandaa kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi  kuokoa maisha huku akisema  taasisi hizo ni pamoja na zinazohusika na huduma ya utafutaji na maokozi, usalama wa wananchi, afya na makazi ya muda na huduma zingine za kijamii.

“Nazikumbusha taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi pamoja na kuimarisha mifumo kama vile usafiri, mawasiliano, nishati na maji kujiimarisha ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa. Taasisi saidizi zina wajibu wa kuwezesha taasisi zenye jukumu ongozi katika kuokoa maisha na mali ili zitekeleze majukumu kwa ufanisi pamoja na kupunguza athari kwa jamii,” Ameeleza.

Aidha amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua kuzuia madhara kufuatia utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2023 kuonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 na kuendelea mpaka Mwezi Januari 2024.

“Historia inaonesha madhara yanayoweza kutokea katika sekta kutokana na uwepo wa El Nino utakaosababisha mvua kubwa ni pamoja na uharibifu wa miundo mbinu mbalimbali, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali. Maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini,”Amebainisha Bw. Mutatebwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.