Mwalimu mkuuu wa Skuli ya Trifonia Protas. Bernardo Nicodemu akimkabidhi msaada wa vitu mbalimbali msimamizi msaidizi wa kituo cha kulelea na kutuniza watoto yatima ZASO Maryam Mohammed wakati walipotembelea kituo hicho na kuwafariji.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Rahma Khamisi Maelezo.
Jamii imeshauriwa kusaidia taasisi zinazoshughulikia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kupata haki zao kama watoto wengine.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka kwa uongozi wa Skuli ya Trifonia ,Msimamizi wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima (ZASO) Shaabani Ali Abdalla amesema watoto hao wanahitaji faraja na kuenziwa kutokana na hali walizokuwanazo.
Amesema vituo vinavyotunza na kusimamia watoto hao vinajukumu la kuwapatia elimu,malazi bora,matibabu na chakula, hivyo aliiomba jamii kuongeza nguvu za kuwalea vyema watoto hao hadi kufikia malengo na kukamilisha ndoto zao za maisha.
Alisema katika kituo hicho wapo watoto wenye fani mbalimbali hivyo wakiendelezwa wataweza kujitegemea na kusaidia watoto wenzao katika siku za baadae .
"Sisi kama taasisi inayosaidia watoto tuna haki ya kuwatunza kwa kuwapatia vitu mbalimbali ikiwemo mahitaji ya skuli kwani wana haki kama watoto wengine" alisisitiza Msimamizi wa Kituo.
Mbali na hayo msimamizi huyo alisema watoto hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa usafiri maalum kwa watoto wanaosoma Skuli za mbali jambo ambalo linawapa usumbufu wanafunzi hao.
Hata hivyo alisema watoto pamoja na uongozi wa kituo hicho umefarajika kutembelewa na wanafunzi na walimu wa skuli hiyo kwani ujio wao umesaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Nae Mkurugenzi wa Skuli hiyo Grace Bernad amesema kwa pamoja wana jukumu la kusaidia watoto hao hivyo uongozi wa skuli ya Trifonia utajitolea kusomesha watoto kumi wa kituo hicho katika skuli yao bila malipo ili kuwapunguzia masafa marefu ya kwenda kutafuta haki yao ya elimu.
Mapema aliwataka watoto hao kuwa na nidhamu ya kuwasikiliza walezi wao na kuwa na bidii ya masomo yao ili kuepusha kuwa tegemezi katika maisha ya baadae.
Nao watoto hao wameushukuru Uongozi wa Trifonia na kuwataka kuendelea kuwatembelea mara kwa mara ili kuimarisha ushirikiano kati yao.
Skuli ya Trifonia ilikabidhi vitu mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho ikwemo mafuta,sukari, unga ,maharage ,mayai na sabuni ikiwa ni mrejesho kwa jamii kutoka kwa skuli hiyo inayotimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.
No comments:
Post a Comment