Habari za Punde

Mhe Othman ziarani Wete

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, leo Jumamosi Oktoba 28, 2023 amefanya Ziara Maalum huko Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, na kushiriki katika harakati mbalimbali za kijamii.

Katika Ziara yake hiyo, Mheshimiwa Othman ambaye yupo kisiwani Pemba kwa Shughuli mbalimbali za Chama na Serikali, ameanza kwa kutembelea Hospitali ya Wete, ambapo amewajulia hali Wagonjwa waliolazwa hapo, akiwemo Bi Viwe Makame Khamis 'Viwe Mkojani'.
Baada ya hapo, Mheshimiwa Othman amefika huko Kipangani na Baghani-Kizimbani Wete, ili kuwatembelea na kuwakagua Wagonjwa na Watu wasiojiweza wakiwemo Bw. Kombo Mbarouk Ali. Na Bi Chumu Nassor Hamad (Shangazi yake).
Aidha Mheshimiwa Othman amefika Baghani-Kizimbani Wete kwaajili ya Kutoa Mkono wa Pole kwa Familia za Marehemu Bi. Mgeni Said Khalfan na Bi. Asha Juma Salim, ambao walifariki dunia hivi karibuni.
Kabla ya hapo, Mheshimiwa Othman amepata fursa ya kuonana na kusalimiana na Kaka yake, Mzee Rashid Hamad Othman, hapo Utaani pia Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Katika Ziara hiyo, Mheshimiwa Othman ameambatana na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiwemo Afisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba, Bw. Khamis Bilal Ali, na Mratib wa ACT-Wazalendo kisiwani hapa, Mhe. Said Ali Mbarouk.
Katika Salamu zake, Mheshimiwa Othman amewatakia Dua Watu hao, pamoja na kuwaombea Rehma Marehemu, na pia kuwatakia subra Wafiwa wote, huku akiwanasihi waendelee kuwa kitu kimoja, hata baada ya kuondokewa na Wapendwa wao.
Wakati wa Ziara hiyo, Mheshimiwa Othman amepata nafasi ya kusalimiana na Wanafunzi na Walimu wa Madrasat Munawwar ya huko Utaani Wete, ambao hatimaye wamemuombea Dua.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Oktoba 28, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.