Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid akimkabidhi sare ya Skuli mwanafunzi Mwanaisha Saidi ikiwa ni sadaka kutoka kwa kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana.
Mwalimu Mkuuu Skuli ya Msingi Bambi Muhammed Ramadhan Mapuri akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wazazi na wanafunzi wa Skuli hiyo kufuatia msaada wa Sare za Skuli uliotolewa na kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana.
Na Fauzia Mussa, Maelezo
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid amewataka wazazi kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha upatikanaji wa elimu na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira bora ya kujisomea.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa Sare za Skuli kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu huko Bambi Wilaya ya Kati Mkoa wa kusini Unguja, Mkuu huyo amesema kufanya hivyo kutasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao walizozitarajia.
Alisema hatua iliyochukuliwa na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ya kuekeza katika sekta ya elimu ni yakupongezwa kwani kutasaidia kuwaweka wanafunzi katika mazingira rafiki ya kujisomea .
“ Kuna baadhi ya wanafunzi wanawacha kwenda skuli kutokana na kukosa mazingira rafiki ya kujisomea ikiwemo kuchanika kwa sare zao hivyo sadaka hiyo itaendea kutimiza ndoto za wanafunzi hao”,alieleza Mkuu huyo.
Mkuu wa Mkoa aliwataka wazazi na walezi kuzitunza na kuzitumia vizuri sare hizo ili kufikia lengo lililokusudiwa pamoja na kuwaomba wadau na wahisani kuwekeza katika sekta ya elimu kwani elimu ni sadaka inayoendelea.
“Sio mnachukua sare mnaenda kuchungia kwa sababu tu ni za msaada ni wajibu kuthamini juhudi hizi zinazochukuliwa na wenzetu za kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira rafiki”, alisistiza Mkuu huyo.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kati Marina Tomas aliwataka wazazi kuacha kuwapa wanafunzi majukumu yasiowahusu na badala yake kuwapatia muda wa ziada kuweza kupitia masomo yao.
Aliwasisitiza walimu kujitahidi kuwasimamia na kuwasomesha vizuri wanafunzi ili kuhakikisha ongezeko la ufaulu linakuwa katika Wilaya hiyo na kutimiza ndoto zao walizotarajia.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Alhaj Abdalla Talib Abdalla amesema Kamisheni ina jukumu la kusimamia haki pamoja na ugawaji wa sadaka na zaka kwa wanaostahi hivyo imeamua kutoa sadaka ya sare za skuli kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu ili wapate kufarijika na kusoma vizuri kama wanafunzi wengine.
Hata hivyo aliwaomba wananchi kutoa sehemu katika mali zao na kuwapa wanaostahiki kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah.
Akitoa neno la shukurani Mwalimu Mkuuu Skuli ya Msingi Bambi Muhammed Ramadhan Mapuri amesema sare ni nyenzo muhimu miongoni mwa nyenzo za kujifuniza hivyo sadaka hiyo ni faraja kubwa kwa wanafunzi na itapelekea kujiamini katika masomo yao.
Hata hivyo aliwataka wadau wa elimu na wenye uwezo kujitokeza kusaidia wanafunzi hao katika mambo mbalimbali ya kuwajengea mazingira rafiki ya kujisomea ikiwemo kufanyiwa ukarabati wa skuli pamoja na kupatiwa vikalio.
Jumla ya wanafunzi 284 wenye mazingira magumu wa msingi na Sekondari katika Skuli ya Bambi wamepatiwa sare za skuli kutoka kwa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar .
No comments:
Post a Comment