Habari za Punde

Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Damas Akagua Ukarabati wa Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam na Wafikia Asilimia 95

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiangalia nyasi zilizopandwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa ziara yake kutembelea na kujionea maendeleo ya ukarabati mkubwa wa uwanja huo.

Na Shamimu Nyaki
Ukarabati wa Awamu ya Kwanza unaoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 95 na asilimia tano zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ndani ya siku tano kuanzia leo.

Akikagua ukarabati huo  leo Oktoba 9, 2023, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema  tayari vyumba vinne vya wachezaji, sehemu ya kuchezea, vyumba vya waamuzi, afya na eneo la video za marejeo (VAR) umekamilika.

" Tayari taa za kisasa 320 za mfumo wa LED zimefungwa na kuna huduma ya mtandao wa bure kabisa kwa ajili ya watazamaji wa mechi ambao tutauzindua kati ya tarehe 17 hadi 19 mwezi huu kabla ya mchezo wa ufunguzi wa African Football League kati ya  Timu ya Simba na Al Alhy ya nchini Misri  tarehe 20,2023 " amesema Mhe. Ndumbaro.

Ameongeza kuwa, katika eneo la watu mashuhuri na sehemu ya wandishi wa Habari kazi iliyobakia ni ndogo ambayo itamalizika ndani ya siku hizo tano akiongeza kuwa mfumo wa sauti uwanjani tayari umerekebishwa.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Kampuni ya  Formula 360, itafunga mfumo wa matangazo kidijitali ambao utaanza kufanya kazi rasmi Oktoba 20, 2023 huku akisistiza kuwa baada ya mchezo huo, ukarabati mkubwa wa awamu ya pili utaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.