Habari za Punde

Balozi wa Norway ahimiza serikali, wadau kuongeza mbinu zaidi kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa Wanawake.

Balozi wa Norway Tanzania, Balozi Tone Tinnes,(kushoto) na Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa alieleza TAMWA ZNZ (kulia) wakielezana jambo wakati wa mdahalo.

BALOZI wa Norway Tanzania, Balozi Tone Tinnes amewataka wadau wa kutetea masuala ya wanawake na uongozi pamoja na ushiriki katika demokraisia kuwekeza katika mbinu za kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake vinavyowakwamisha kufikia malengo ya kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali.

Balozi Tinnes amesema hayo wakati aliposhiriki mdahalo wa kitaifa wa wadau wa kutetea masuala ya wanawake na uongozi pamoja na ushiriki wao katika demokrasia Zanzibar ulioandaliwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar, (ZAFELA na Jumuiya ya utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Tanzania.

Akizungumza kwenye mdahalo huo uliolenga kujadili hali ya wanawake na uongozi Zanzibar katika siku 16 za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto, alisema ajenda ya usawa wa kijinsia ni  muhimu kutiliwa mkazo na wadau wote ili kuhakikisha inafikiwa bila kuwa na vikwazo vya aina yoyote.

Alieleza, “ajenda ya 50/50 ni ajenda ya kidunia,  hivyo ni muhimu kuangalia jinsi gani kama wadau tunaweza kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake ili waweze kushika nafasi za uongozi."

Alisema midahalo ya kujadili nafasi ya wanawake na vikwazo vinavyowakabili navyo katika uongozi ni muhimu katika kuwajengea uwezo wanawake kujitayarisha hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Tnzania wa mwaka 2025.

"Majukwaa kama haya ya kujadili masuala ya wanawake na uongozi ni muhimu hasa tunapojipanga kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025, na kuna changamoito nyingi hasa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia," alieleza Balozi Tinnes.

Aidha Balozi huyo alieleza kuguswa na juhudi za TAMWA Zanzibar  za kutetea haki za wanawake katika kupinga vitendo vya ukatili Zanzibar, na kueleza kuwa Serikali ya Norway itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kufikia lengo la usawa wa kijinsia.

Balozi Tinnes alisema, “ujumbe mkuu wa mwaka huu umetushajihisha kuwekeza katika kupinga udhalilishaji wa kijinsia, na sisi ubalozi wa Norway, tumewekeza katika kusapoti TAMWA Zanzibar kwenye kuwawezesha wanawake kuanzia mashinani.”

Katika hatua nyingine Balozi Tinnes alibainisha kufurahishwa na utayari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwa mstari wa mbele kukuza kwa vitendo ushiriki wa wanawake katika nafasiza uongozi.

"Nafurahi kuona viongozi wakuu wa serikali kufika hapa kwani inaonesha kuwa kama nchi wanawekeza katika kukuza usawa wa kijinsia, ikiwemo  nafasi na uongozi Kwa wanawake” alifahamisha Balozi huyo.

Mapema Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Anna Athanas Paul, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mkakati muhimu wa kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali kwa mjibu wa mikataba ya kikanda na kimataifa.

Alisema, “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendela kutekeleza mikakati muhimu ya kuwawezesha wanawake ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na ya kikanda, na nafasi hizi si nafasi za upendeleo bali ni kuziba nafasi na mapengo ya usawa wa kijinsia iliyopo.”

Nae Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar (WEMA), Khamis Abdullah Said alizitaka taasisi za Serikali na kiraia kuanza kutekeleza mkakati wa usawa wa kijinsia kwa kuzingatia uwiano sawa katika nafasi zote za uongozi kwenye ngazi mbalimbali.

Alisema, "kuna haja kwa taasisi za serikali na zisizo za serikali kuzingatia uwiano wa jinsia katika nafasi za uongozi, mfano mzuri ni Wizara ya elimu, mkurugenzi mtendaji, mkurugenzi elimu mbadala, muhasibu, mkaguzi mkuu na mkurugenzi wa kitengo elimu ya juu haWA wote ni wanawake."

Alisema wizara hiyo ipo katika hatua za kurekebisha sera ya elimu, hivyo atahakikisha utekelezaji wake utazingatia na kuaksi ajeng=da ya usawa wa kijinsia kwa kutoa fursa sawa kwa wote.

“Hivi sasa  tunarekebisha Sera ya elimu, na mimi nitahakikisha inazingatia uwiano wa kijinsia. Lakini pia tunatekeleza kwa vitendo ajenda hii, kwani wizara ya elimu safu ya uongozi imezingatia sana nafasi za wanawake, kwa mfano vitengo vingi vya wizara vinaongozwa na wanawake,” alieleza katibu mkuu WEMA.

Mapema Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa alieleza TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wengine waliandaa mdahalo huo kwa lengo la kuongeza hamasa kwa wanawake kutokata tamaa na badala yake wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zinapojitokeza.

Alisema wanawake katika siasa wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwemo udhalilishaji hasa mwanamke anapoonekana kuwa ni tishio kwa wanaume.

Alifahamisha, ‘lengo la mdahalo huu ni kuwashajihisha wanawake wenyewe katika kugombea nafasi za uongozi. Pia kuona ni jinsi gani wadau mbalimbali wanaweza kusaidia kuondoa vikwazo kwa wanawake katika uongozi ikiwemo viongozi wa dini, polisi, ZAECA na wengine."

Mwakilishi Jimbo la Konde Pemba, Zawadi Amour, kupitia Chama cha Mapinduzi, akichangia mada aliwasihi wanawake kujiamini na kutokatishwa tamaa na vikwazo wanavyowekewa na badala yake wavitumie kama ngao ya kufikia ushindi wao.

"Kujiamini ni ngao ya kumvusha mwananmke na kuweza kutimiza malengo yake kwenye uongozi, ni lazima kuwa na malengo bayana  na upambanie kuyatimiza," alieleza, mwakilishi Jimbo la Konde, Pemba.

Mdahalo huo wa kitaifa umehudhuriwa na viongozi kutoka taasisi za kiserikali na asasi za kiraia, vyama vya siasa, wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, viongozi wa dini, vijana wa kike na wanawake kutoka maeneo mbalimbali na kupata fursa ya kujadili mbinu wezeshi za kuwasaidia wanawake kushika viti vya uongozi ifikapo uchaguzi 2025 pamoja na kubainisha njia za kuvunja vizuizi na kufungua fursa zaidi kwa wanawake na vijana.

Balozi wa Norway Tanzania, Balozi Tone Tinnes, akizungumza katika mdahalo wa kitaifa wa wadau wa kutetea masuala ya wanawake na uongozi pamoja na ushiriki wao katika demokrasia Zanzibar ulioandaliwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar, (ZAFELA na Jumuiya ya utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Tanzania.
 Balozi wa Norway Tanzania, Balozi Tone Tinnes (kushoto), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Anna Athanas Paul(kulia) wakizungmza wakati wa mdahalo.
Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar (WEMA), Khamis Abdullah Said akizungumza kwenye ufunguzi wa mdahalo.

 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Anna Athanas Paul akichangia wakati wa mdahalo.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.