Habari za Punde

Wadau Jitokezeni ‘Kuisapoti ’ Stars AFCON 2023 – Mhe. Ndumbaro

Na Brown Jonas - WUSM

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro ametoa rai kwa wadau wa Soka nchini kujitokeza kwa wingi katika kuiunga mkono timu ya Taifa ya mpira wa miguu Taifa stars inayojiandaa na Mashindano ya Afcon yatakayofanyika mapema mwezi Januari 2024 Nchini Ivory Coast.

Mhe. Ndumbaro amesema hayo leo desemba 30, 2023 Jijini Dar Es Salaam kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo ameeleza umuhumi wa mashabiki katika kuiwezesha Stars kufanya vizuri.

“Kwanza niwashukuru sana kwa siku za hivi karibuni hamasa imekua kubwa sana, sasa tunaomba hamasa iendelee hasa tunapoelekea mashindano ya Afcon tutumie mitandao ya kijamii kuisemea vizuri timu yetu ili kuipa hamasa”

Aidha Mhe. Ndumbaro amesema kuwa Januari 30, 2024 wizara kwa kushirikiana na Shirikisho la soka nchini TFF itafanya harambee ya kuichangia Taifa Stars ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema ni vyema wadau kuiga mfano wa Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika “kuisapoti Stars” kama amabavyo huwa anafanya.

Taifa Stars inatarajia kuondoka hivi karibuni kuelekea nchini Misri kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi pamoja na kucheza mechi za kirafiki kabla ya kuelekea nchini Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.