Habari za Punde

Mafanikio ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Yaelezewa Katika Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Mhe.Harusi Said Suleiman akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maendeleo ya Ofisi hiyo katika miaka 60 ya Mapinduzi huko Karume house Mjini Unguja

Na Rahma Khamis Maelezo.     5/1/2024.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman amesema Serikali imefanikiwa kujenga Mtambo wa kusafisha Maji machafu katika eneo la Msingini Chakechake Pemba ili kudhibiti uchafuzi wa Mazingira.

 

Ameyasema hayo wakati akielezea Mafanikio na Mikakati ya Ofisi hiyo, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi.

 

Amesema Serikali imejenga Msingi wa kupitishia Maji ya Mvua, wenye urefu wa mita 100 katika eneo hilo sambamba na kuondosha Tani 360 za kemikali hatarishi zilizomaliza muda wa matumizi.

 

Amefahamisha kuwa Serikali imeanzisha Tume ya Ukimwi Zanzibar kwa lengo la kukinga na kudhibiti masuala ya Ukimwi ili kuzuia maambukizi mapya kwa wengine.

 

Ameongeza kuwa Tume kwa kushirikiana na Wadau mbalimali imeanza kupunguza Unyanyapaa na kuweka Mikakati madhubuti ya kudhibiti maambukizi yasiongekezeke.

 

Akizungumzia kuhusu Watu Wenye Ulemavu amesema Serikali imefanikiwa kutoa jumla ya Vifaa saidizi 186, ikiwemo Fimbo, Vigari, Viti na Vifaa vyengine kwa ajili ya usaidizi.

 

Aidha ameeleza kuwa jumla ya Vikundi 11 vya Watu wenye Ulemavu vimewezeshwa na kupatiwa Mikopo ili kuweza kujiendeleza na kujiunua kiuchumi ambapo Serikali inatarajia kuongeza Idadi ya vikundi vyengine kadri hali ya uwezo itakaporuhusu.

 

Hata hivyo amewaomba Wananchi kushirikiana na Masheha katika maeneo yao kwa kutoa taarifa sehemu husika ili Serikali iweze kudhibiti matumizi ya Dawa za kulevya nchini.

 

Sambamba na hayo Mhe. Harusi amebainisha kuwa Serikali imedhibiti matumizi ya Mifuko ya plastic ambayo ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa Mazingira hivyo amewataka Wananchi kutunza Mazingira ili kuweza kuweka Mji safi.

 

Hata hivyo Waziri huyo amebainisha kuwa wanatarajia kuifanya Zanzibar kuwa ya kijani kwa kuendeleza Miradi ya kiuchumi, kuhifadhi Mazingira, kuimarisha zoezi la ufatiliaji na kusimamia masuala ya Watu Wenye Ulemavu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.