Na Happiness Shayo
Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetia saini
mikataba sita ya uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori
(Special Wildife Investment Concession Areas - SWICA) yenye thamani ya dola za
Kimarekani milioni 278, sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 696 kwa ajili ya
kuendeleza miundombinu ya utalii katika maeneo sita ya uwekezaji.
Maeneo hayo ya uwekezaji ni Pori
la Akiba Mkungunero Mkoani Dodoma, Mapori ya Akiba ya Ikorongo na
Grumet Mkoani Mara pamoja na Mapori ya Akiba ya Maswa Kimali, Maswa Mbono na Maswa
Kaskazini yaliyopo Mkoani Simiyu.
Hafla ya utiaji saini imefanyika
leo Januari 3, 2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema utekelezaji
wa SWICA utaongeza utalii na mapato katika maeneo yatakayofanyiwa uwekezaji
huo, hali itakayochangia kwa kiasi kikubwa kutekeleza lengo la kuongeza idadi
ya watalii kutoka milioni 1.5 mwaka 2021/2022 hadi milioni 5 mwaka 2025/2026.
“Uwekezaji huu utaiingizia
Serikali mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 314 katika
kipindi cha miaka 20 ya uwekezaji sawa na dola milioni 16 kwa mwaka (sawa na
shilingi za kitanzania bilioni 40). Mafanikio haya yanatokana kwa kiasi kikubwa
na utangazaji utalii kupitia Filamu ya “Tanzania- The Royal Tour” iliyoandaliwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”
amesisitiza Mhe. Kairuki.
Ameongeza kuwa miongoni mwa
manufaa mengine yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo ni kuimarika kwa
uhifadhi, utafiti na kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka maeneo ya
uwekezaji ambapo takribani dola za Kimarekani milioni 50, sawa na shilingi za
kitanzania bilioni 125, zitatumika kufadhili Miradi ya Maendeleo ya Jamii
katika kipindi cha miaka 20 ya uwekezaji.
Aidha, amezipongeza kampuni za
Bushman Safari Trackers Ltd, Grumeti Reserves Ltd, Mwiba Holdings Ltd na Megallan
General Trading LLC kwa kufanikiwa kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji ya Bushman Safari
Trackers Ltd, Talal Abood amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi za kukuza utalii na
kushirikisha sekta binafsi kwa lengo la kukuza uchumi wa Tanzania.
“Tunaishukuru Wizara ya Maliasili
na Utalii kwa ushirikiano na tunaahidi kwamba tunaenda kutekeleza hili jambo
kwa ufanisi mkubwa na uharaka mkubwa ili
kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya
Sita kwenye kutekeleza Sera ya Utalii” amesema Bw. Talal.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), Katibu Mkuu, Wizara
ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja
Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na
maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali
wa uhifadhi.
No comments:
Post a Comment