Habari za Punde

Waumini wa Kiislamu Wametakiwa Kuishi kwa Maadili ya Kizanzibari, Mila, Silka na Desturi Ili Kupata Vizazi Bora

Wazanzibari na Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kuishi kwa kufata maadili ya kizanzibari, Mila, Silka na Desturi ambazo wazazi wetu walizifata ili kupata vizazi bora vya baadae.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid NGAVA uliopo KINYASINI Wilaya ya Kaskazini “A”  mara baada ya kumaliza  Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema wazazi na walezi wanapaswa kusimamia maadili kwa watoto wao pamoja na kufuata nyayo za wazee waliopita ili kuondosha mambo mbali mbali ambayo yanasababisha kuwepo kwa vitendo  viovu kwa vijana wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni wajibu wa kila Mzanzibari kupiga vita suala la udhalilishaji, madawa ya kulevya sambamba na kuwataka wakaazi wa kinyasini na vijiji jirani kurudi katika mila, silka na utamaduni wa kizanzibari ili kuweza kupata kizazi chenye maadili mema.

Alhajj Hemed amesema waumini wanapaswa kuzitumia nyumba za ibada kwa kufanya ibada pamoja na kutafuta suluhu ya changamoto mbali mbali zinazowakabili ikiwemo suala la  mmong’onyoko wa maadili katika jamii zetu kwa kufuata maandiko matakatifu na fatwa za wanazuoni mbali mbali.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka maimamu wa misikiti pamoja na waumini kujenga  utamaduni wa kujiombea dua na kuiombea dua Nchi yao ili iweze kuondokana na majanga mbali mbali ikiwemo janga la udhalilishaji ambalo limekuwa likiishushia hadhi nchi yetu na kuwapa wakati mgumu wanawake na watoto ambao ndio wahanga wakubwa wa udhalilishaji.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Maalim ALI KHAMIS FOUM  amewaomba waumini wa Dini ya Kiislam kuendelea kushikamana pamoja katika kutenda mema na kukatazana maovu ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu na ni kichocheo cha uvunjifu wa maadili katika jamii zetu.

Amesema kuwa wazazi na walezi wana jukumu la kufatilia tabia za watoto wao na kushikamana nao katika kuwafundisha yaliyo mazuri kwa dunia na akhera yao jambo ambalo litawezesha kupata vizazi bora vinavyompendeza (S.W)

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe..05.01.2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.