Habari za Punde

Tigo Zantel Kwa Kushirikiana na Laina Finance Limited Yazindua Huduma ya Pata Dawa Kupitia Simu ya Mkono

Mufti Mkuu wa Zanzibar Shekh Saleh Omar Kaabi, alisema mfumo huo wa msaada ulioanzishwa na kampuni hiyo ni jambo zuri kwani Mwenyezimungu ameumba waja wake ili waweze kusaidiana katika mambo mbalimbali.
Afisa Mkuu wa Tigo Pesa kutoka kampuni ya Tigo Zantel, Angelica Pesha, alisema kampuni hiyo inategeneza historia kwani huduma ya Pata dawa ni huduma ya kidijitali ambapo kwa Tanzania ni nchi ya kwanza kwa Afrika Mashariki kwa ujumla.

WIZARA ya Afya Zanzibar, imeitaka kampuni ya simu ya mkononi Tigo Zantel na Laina Finance Limited kuhakikisha wanafuata misingi ya faida inayozingatia ubinaadamu na sio kukomoa wananchi katika huduma ya pata dawa.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hassan Khamis Hafidh, alieleza hayo wakati akizindua huduma hiyo ya Pata Dawa kupitia simu ya Mkononi Tigo Zantel kwa kushirikiana Laina Finance Limited katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege.


Alisema mfanyabiashara biashara mara nyingi amekuwa akinunua rahisi na kuuza ghali hivyo aliwasisitiza kuacha kufanya hivyo kwani watanzania wakiwemo wazanzibari ni wangonge na uislam unataka kutoka kwenye riba na kwenda kwenye faida.


“Watanzania wakiwemo wazanzibari ni wanyonge hivyo msije mkawakomoa ni lazima kufuata misingi ya faida pia muweke wazi pale inapomnunulia mtu dawa au kitu chochote basi kumwambia mapema faida yake kuwafahamisha mwananchi mapema na sio faida inayokomoa bali izingatie ubinaadamu kwani nchi yetu ni masikini na watu wake ni masikini,” alisisitiza.


Aidha alisema huduma hiyo ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwani wananchi wengi ni wangonge hivyo ni lazima kusaidiana katika mambo mbalimbali.


“Jambo la kununua dawa katika njia ya tigo pesa ni huduma muhimu kwani wanananchi wengi ni wanyonge hiyo ni hatua nzuri na jambo jema,” alisema.


Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada anazozichukua katika kuimarisha huduma bora ya afya ikiwemo majengo na upatikanaji wa vifaa tiba na kinga ikiwemo dawa.


Mbali na hayo aliomba kutekeleza ombi la mufti kwa kutoa mwezi mmoja mwananchi kulipa kwa mwezi mmoja na sio siku 10 atakapotumia huduma hiyo. 


Alipongeza Tigo Zantel na Lainner Finness kuja na program hiyo ya pata dawa ambayo itamuwezesha mtu kupitia mitandao kununua kwa kutumia manunuzi ya kislam yenye lengo la kuwasaidia wananchi wanyonge ambalo linakwenda katika sharia ya kislam na sharia ya riba.


Sambamba na hayo aliwataka pia kubuni huduma nyengine mbalimbali ambazo zitaweza kuwasaidia wanadamu ambazo wanazihitaji katika maisha yao ya kila siku.


Naye Mufti Mkuu wa Zanziba,r Shekh Saleh Omar Kaabi, alisema mfumo huo wa msaada ulioanzishwa na kampuni hiyo ni jambo zuri kwani Mwenyezimungu ameumba waja wake ili waweze kusaidiana katika mambo mbalimbali.


Alisema miongoni mwa mambo muhimu anayohitaji binaadamu ni msaada mkubwa wa afya ukiachia nyanja za elimu uchumi na nyengine.


"Mtu akiwa mnyonge wa afya basi atafika katika hali ngumu na anahitaji kusaidiwa na wenzetu mmekuja na zana hii ya pata dawa ili kuwasaidia wananchi wa Unguja na Pemba," alibainisha.


Alipongeza kampuni hiyo kuja na jambo hilo ambalo halina riba kwani Mwenyezimungu amekataza jambo hilo lakini kuuza na kununua biashara jambo hilo limekubalika.


"Kumuwezesha mtu kupata dawa na afya yake ikaimarika basi itakuwa umemsaidia mtu huyo na jambo zuri ambalo linatakiwa katika uisalam kwani Mwenyezimungu analifurahia na atakuwa mtu ambae anawanufaisha wanaadamu wenzake huyo ni mtu bora," alibainisha.


Shekh Kabbi alitumia fursa hiyo kuipongeza Tigo Zantel kwa uamuzi huo wa kusaidiana na kushauri watu na kampuni nyengine kutafuta mbinu za kuwasaidia wengine katika nyanja mbalimbali ili kuona watu wanaendelea kupata maisha bora kama watu wengine bila ya matatizo.


Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Tigo Pesa kutoka kampuni ya Tigo Zantel, Angelica Pesha, alisema kampuni hiyo inategeneza historia kwani huduma ya Pata dawa ni huduma ya kidijitali ambapo kwa Tanzania ni nchi ya kwanza kwa Afrika Mashariki kwa ujumla.


Alisema tayari wameshasajili maduka ya dawa na hospitali mbalimbali kwa Unguja na Pemba na mteja akienda katika maduka hayo na amepata dharura na hana uwezo wa fedha katika akaunti yake ya tigo pesa basi anaweza kuhudumiwa kupitia huduma hiyo ya pata dawa na tigo pesa.


Alisema ni matarajio yao huduma hiyo italeta tija kwa wananchi wa Zanzibar katika kuwapatia dawa kupitia huduma hiyo ambayo inawapa nafasi wateja kununua kwa njia ya kislam na kulipa fedha kwa mujibu wa bei aliyouziwa bila ya kuwa na riba.


“Lengo letu ni kuwawezesha wananchi masikini kupata huduma katika kipindi cha shida na pesa zije baadae kwani malengo ya kampuni yetu ni kutoa huduma bora kwa wananchi pale wanapokuwa na shida mbalimbali za kimaisha za kifedha ili waweze kujihudumia na kuweza kulipa baadae,” alisema.


Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Sharia Laina Ahmed Jabir, alisema hivi sasa Zanzibar inabadilika kutoka kwenye mifumo ya riba na kwenda kwenye mifumo ya faida ambapo serikali imekuwa ikiunga mkono katika mambo hayo.


Aliahidi kwamba muamala huo hautakuwa na tatizo kwani lipo katika sheria za kislamu na kuiomba serikali Zanzibar kuendelea kushirikiana na sekta binafsi kwani wapo tayari kujitolea katika kuendeleza misingi ya fedha ya kislaam hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.