Habari za Punde

Wazazi na walezi wametakiwa kuwalea watoto wao katika malezi yaliyo bora ili kukua katika maadili mema na kuirejesha Zanzibar iliyoachwa na wanazuoni waliopita kabla yao.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid SALAMI MLANDEGE  mara baada ya kumaliza  Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema wazanzibari na waumini  wana wajibu wa kuwalea watoto wao katika maadili mazuri kama waliokuwa nayo wanazuoni waliopita kwani kufanya hivyo watalisaidia taifa kupata viongozi walio wazuri na wenye hofu ya Mwenyezimungu katika ufanyaji wao wa kazi.

Alhajj Hemed amesema wapo vijana wa kizanzibari wamenajishughulisha na vitendo viovu ikiwemo udhalilishaji, matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na wizi hivyo, ni vyema jamii kuungana pamoja kudhibiti vitendo hivyo ikiwemo kusaidiana katika malezi.

Mhe.Hemed amesema kuwa wakati uliopo kwa sasa ni lazima wazazi kuhakikisha wanawasimami vijana wao ili kurejesha mila na silka za kizanzibari zilizokuwepo kabla yao jambo ambalo litairejeshea sifa Zanzibar ambayo ndio chimbuko la wanazuoni mbali mbali wa dini ya kiislamu ukanda wa Afrika Mashariki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kujitathmini katika malezi kwa vijana wao anaowalea kwani kufanya hivyo kutasaidia kupata wanazuoni watakaoweza kuisimamia nchi pamoja na dini kwa ujumla.

Sambamba na hayo  Alhajj Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar na watanzania kwa ujumla kuzidi kuwaombea dua viongozi wao na kuacha tofauti zilizopo  baina yao ili kuiacha nchi yenye neema kwa faida ya vizazi vya sasa na vya baadae.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Maulana Sheikh  ABUUBAKAR MUBARAQ  amewataka waumini wa Dini ya Kiislam kusameheana na kusafiana nia kwa kila walilokosana ili kuweza kujitakasa kwa Allah (S.W) na kuingia katika Mwezi mtukuru wa Ramadhani unaotarajiwa kuifia hivi karibuni ikiwa wametakasika baina yao.

Amesema kuwa waislamu ni lazima kushirikiana na kuamrishana mema sambamba na kukatazana mabaya ili kujiweka karibu na Allah (S.W) na kufikia lengo la kuumbwa mwanadamu hapa duniani.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe..23.02.2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.